Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), hivi sasa lina ukwasi wa Shilingi Trilioni 5.14, aidha linalipa kodi zote za Serikali kiasi cha Shilingi bilioni 35 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah, ameyasema hayo akitoa wasilisho lake kwa ujumbe kutoka Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) uliofanya ziara Jijini Dodoma ya siku moja kubadilishana ujuzi wa kiuendeshaji na NHC.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amesema, NHC inapata faida ya zaidi ya Shilingi bilioni 135 kwa mwaka.
Baada ya wasilisho hilo, ujumbe huo kutoka Zanzibar ulipata fursa ya kufanya ziara ya kikazi kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na NHC kama mkandarasi na pia ile ambayo NHC inatekeleza kama miradi yake ya ndani.
Awali akizungumza akiukaribisha uongozi wa ZHC, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi wa NHC, Dorothy Mwanyika amesema ushirikiano ulioanzishwa baina ya Taasisi mbili hizo ni jambo lenye manufaa makubwa kwa taifa na hivyo taassisi hizo hazina budi kufanya tathmini za mara kwa mara za maendeleo ya ushirikiano. Hii itasaidia kutambua maeneo ya mafanikio na changamoto na kutoa fursa ya kurekebisha mwelekeo inapohitajika. Ziara hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa ushirikiano waliousaini miezi kadhaa iliyopita Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Zanzibar ( ZHC), Abdallah Mwinyigogo, amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa ushirikano wake tangu kuanzishwa kwake na kwamba ushirikano huo umejenga umoja na utayari wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa mafanikio zaidi ya siku zijazo.
Serikali zote mbili kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mashirika hayo yanajengewa uwezo wa kutosha ili kuendelea kutekeleza miradi bora ya makazi kwa ajili ya ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.