Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Februari 12, 2024 ametoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari Ofisini kwake kuhusu kuahirisha ziara yake ya kukagua na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya zote za Mkoa huo ambayo ilipangwa ianze kufanyika leo Februari 12, 2024 Wilaya ya Temeke ili kuungana na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, familia na Watanzania wote kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Edward Ngoyai Lowassa
Akiongea na waandishi wa Habari RC Chalamila amesema kwa kuwa msiba wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa upo DSM hivyo Mkoa umejipanga vizuri katika nyanja zote ikiwemo Usalama na uratibu wa wageni mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye mratibu mkuu wa msiba huo.
Aidha RC Chalamila amesema siku ya kesho Februari 13, mwili wa marehem Edward Lowassa utaagwa katika viwanja vya karimjee Ilala ambapo ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutumia siku hiyo kuja kwa wingi kumuaga mpendwa wetu, kiongozi wetu, Mzee wetu Hayati Edward Lowassa.
Vilevile Februari 14, 2024 mwili utapelekwa katika kanisa la Azania Front kwa ajili ya Ibada, na Februari 15, 2024 mwili wa marehem utasafirishwa kuelekea nyumbani Monduli- Arusha ambapo maziko yanatarajiwa kufanyika Februari 17, 2024 ambayo yataongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sambamba na hilo RC Chalamila ametangaza tarehe ya kuanza ziara yake ambapo amesema ziara hiyo itaanza rasmi Februari 19, 2024 Wilaya ya Temeke Jimbo la Mbagala tarehe 20/02/2024 Jimbo la Temeke, Wilaya ya Kinondoni tarehe 21/02/2024 Jimbo Kawe tarehe 22/02/2024 Jimbo la Kinondoni, Wilaya ya Ubungo tarehe 23/02/2024 Jimbo la Ubungo tarehe 24/02/2024 Jimbo la Kibamba, Wilaya ya Kigamboni tarehe 26-27/02/2024 na Wilaya ya Ilala tarehe 28/02/2024 Jimbo la Ilala, tarehe 29/02/2024 Jimbo la Ukongo na kuhitimisha tarehe 01/02/2024 katika Jimbo la Segerea