Anthony Mtaka Mkuu wa mkoa wa Njombe ambaye amekuwa akizipa. Msukumo mkubwa wa kambi za kujisomea ili kuwandaa wanafunzi kwa mitihani yao ya mwisho na kuongeza ufaulu kwa kiwango kikubwa katika maeneo yote ambayo amekuwa kiongozi.
……………………..
Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Mwanafunzi anapaswa kutenga muda wa kutosha wa kujisomea ili yale anayofundishwa darasani na walimu wake yaendelee kukaa katika ubongo wake na hatimaye aweze kufaulu vizuri katika masomo. Bila kujisomea hakuna kufaulu kwa mwananfunzi, na ndiyo maana wanafunzi wanashauriwa kuwa na ratiba zao binafsi za kujisomea achilia mbali ratiba za vipindi vya madarasani zilizopo shuleni.
Ipo changamoto kwa wanafunzi wengi hasa wa shule za msingi na sekondari za kutwa kushindwa kujisomea ipasavyo kutokana na uhuru mkubwa walionao pindi wanaporejea nyumban baada ya kumalizika vipindi vya shuleni. Changamoto hii inachangia sana kushuka kwa ufaulu kwa wanafunzi wanaosoma shule za kutwa na ndiyo maana juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, asasi za kiraia, wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla kuhamasisha ujenzi wa mabweni katika shule za msingi na sekondari.
Kwa kuwa gharama ni kubwa katika kutekeleza azma hii ya ujenzi wa mabweni, serikali inatekeleza suala hili kwa awamu baada ya awamu kulingana na upatikanaji wa raslimalifedha huku juhudi za kuhakikisha wanafunzi wanapata muda wa kutosha wa kujisomea zikiendelea kufanyika. Njia mojawapo inayotumiwa na serikali kupitia uongozi wa ofisi za elimu za mikoa na wilaya ni kuanzisha kambi za kunisomea ili kuwapa wanafunzi muda wa kutosha wa kujisomea. Na hili linafanyika hasa kwa wanafunzi wanaosoma madarasa yenye mitihani ya Taifa kama vile Darasa la Saba, Kidato cha Pili, Nne na Sita.
Kambi za kujisomea ni wasaa wanaoupata wanafunzi kukaa shuleni muda wote kama ambavyo wanafunzi wa bweni wanavyoishi. Katika kambi hizo, wanafunzi huishi kwa kufuata na kuzingatia taratibu zote zinazoongoza shule za bweni. Wazazi na walezi hushiriki kwa kuchangia chakula kitakachotumika kulisha watoto wao na kuwapa watoto wao mahitaji muhimu kama mafuta ya kujipaka, sabuni na fedha kidogo za kujikimu. Hivyo, kambi za kujisomea huwaandaa wanafunzi kuanza kuzoea maisha ya bweni na hii huwasaidia kuendana na mazingira ya bweni pindi wanapojiunga na shule za bweni baadaye.
Wanafunzi wanaokaa katika kambi hizi, hupata muda wa kutosha wa kujisomea hasa muda wa jioni na usiku, kwani mazingira ya kambi huwalazimu kujisomea. Kutokana na wanafunzi kukosa muda wa kuzurula mitaani na usimamizi thabiti wa walimu katika kambi za kujisomea, wanafunzi hulazimika kujisomea zaidi, hali inayowasaidia kujifunza vitu vingi na hatimaye kufikia malengo yao ya kufaulu mitihani. Mwanafunzia awapo kambini, haruhusiwi kulala bwenini wakati wenzake wakijisomea kama hana sababu ya msingi kama vile kuumwa. Lakini ni rahisi kwa mwanafunzi awapo katika mazingira ya nyumbani kwako kulala bila kujisomea hata kama hana sababu ya msingi inayomsababisha kushindwa kujisomea.
Kambi za kujisomea pia hutoa uhuru kwa wanafunzi kujisomea muda wowote na kwa utulivu mkubwa. Licha ya wanafunzi kuwekewa ratiba ya kujisomea nyakati za usiku, lakini bado mwanafunzi ana uhuru wa kuendelea kujisomea kwa kadri ya uwezo wake pindi muda wa wanafunzi wote kujisomea unapokwisha. Lakini pia mwanafunzi anao uhuru wa kulala na kuamka usiku kuendelea kujisomea kabla ya kukucha. Katika mazingira haya, mwanafunzi hujikuta akisoma katika hali ya utulivu mkubwa na kuingiza maarifa mengi kupitia madaftari na vitabu anavyojisomea. Mazingira haya ni adimu sana kupatikana katika nyumba nyingi kwa wanafunzi wanaosoma kutwa.
Faida nyingine ya kambi za kujisomea ni kumsaidia mwanafunzi kuchangamana na wenzake wakati wa kujisomea. Ni muhimu kwa mwanafunzi kusoma na wenzake ili kushirikishana uelewa katika mada mbalimbali za masomo yao. Wakati mwingine kutokana na umbali baina ya makazi ya wanafunzi, inakuwa ngumu kwao kusoma kwa pamoja. Kupitia kambi za kitaaluma, wanafunzi huweza kuchangamana na kujifunza kwa pamoja miongoni mwao. Kutokana na ukweli kuwa uelewa wa wanafunzi unatofautiana kati ya mwanafunzi mmoja na mwingine, wanaposoma pamoja ni njia mojawapo ya kusaidiana wao kwa wao.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.