Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akisalimiana na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC), Bi. Chidi Blyeden, walipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo kuhusu namna Tanzania itakavyotekeleza na kunufaika na mpango wa ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi (Threshold Programs), mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo, Jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza na Mwakilishi wa Tanzania wa Mradi wa MCC Dkt. Hamisi Mwinyimvua
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-dar es Salaam
………………….
Na Benny Mwaipaja, DSM
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameishukuru Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC) kwa kuiteua Tanzania kuwa moja ya nchi zilizoko kwenye mpango wa kunufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi.
Dkt. Nchemba amesema hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo la Changamoto za Milenia-MCC, ukiongozwa na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bi. Chidi Blyeden.
Aliueleza ujumbe huo kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kusimamia uchumi wake, masuala ya utawala bora, haki za binadamu, demokrasia, na kwamba imetekeleza kwa kiwango kikubwa vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo ili nchi iweze kunufaika na mpango huo.
Dkt. Nchemba aliishukuru MCC kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi ambapo kupitia Mradi wa Changamoto za Milenia uliotekelezwa nchini kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2008 hadi 2013, uliiwezesha Tanzania kupata dola za Marekani 698 milioni, zilizotumika kutekeleza miradi katika sekta za usafirishaji, nishati na maji.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameituliza nchi kisiasa, na kuwa na nia ya dhati ya kuituliza nchi kwa kuruhusu masuala ya kisiasa kufanyika kwa uwazi na hata hii si tu kwa ajili ya kutekeleza vigezo vya taasisi yoyote bali ni nia yake ya dhati ya kulinda uhuru wa watu” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), Bi. Chidi Blyeden, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuimarisha masuala ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu chini ya utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua iliyolifanya Shirika lake kurejesha ushirikiano na Serikali.
Bi. Blyeden alieleza kuwa Wataalam kutoka MCC wanaendelea na mijadala na wataalam wa Serikali ili kuharakisha kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo ambao matokeo yake hapo baadae utaiwezesha Marekani kurejesha mradi wa Changamoto za Milenia (MCC-Compact) ambao utakuwa na lengo la kusaidia nchi kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
Mwezi Desemba mwaka 2023, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ilizichagua Tanzania na Philippines, kama wabia wake katika kuandaa programu za awali (threshold programs) zitakazolenga katika mageuzi ya kisera na kitaasisi ambazo nchi hizi zinaweza kuyafanya ili kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Bodi hiyo ya MCC ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania na Ufilipino, kuonesha dhamira mpya ya kusukuma mbele mageuzi muhimu ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kupambana na rushwa.
Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ni shirika huru la Serikali ya Marekani linalojielekeza kupunguza umaskini duniani kupitia ukuaji wa kiuchumi, kwa kutoa ruzuku na misaada ya muda maalum kwa nchi zinazokidhi viwango na vigezo thabiti vya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na kuheshimu haki za kidemokrasia.