Na Sophia Kingimali
CHUO cha ufundi Stadi Furahika kipo mbioni kuanza kutoa elimu kwa kiwango cha Diploma kwa wanafunzi wanaochukua kozi mbalimbali chuoni hapo ikiwamo Hoteli, Umeme, Bandari, Ualimu wa Awali na Tiketi za Ndege huku kikianzisha kozi mpya ya ufundi mabomba.
Hayo yamebainshwa na Mkuu wa Chuo hicho Dk. David Msuya wakati wa mahafari ya 19 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Februari 10, 2024 ambapo wahitimu 66 wamehitimu masomo yao kwa ngazi ya cheti.
“Tunashukuru kuona chuo chetu kinapanda hadhi kutokana na kuwa katika mchakato wa kuanza kutoa kiwango cha Diploma kwa kozi mbalimbali zinazofundishwa hapa chuoni na usajili wetu nao unahama kutoka VETA na kuhamishiwa Nacte, kwetu ni jambo la furaha na kuishukuru Serikali yetu pendwa chini Rais wetu Dk. Samia kwa ushirikiano ambao wanatupa,” amesema.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafari hayo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Alhaji Sultan Said ‘Side’, ambaye aliwakilishwa na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Mtiti Mbassa, amewataka wahitimu hao kuwa na nidhamu na kutokuwa na vitendo vya kihuni wanapokwenda kwenye mazoezi ya vitendo.
Amesema jambo hilo litasaidia kufanikiwa kupata kazi kwa haraka na kuwa mabalozi wazuri wa Chuo cha Furahika ambacho kimsingi ni kama kinatoa elimu bure kwa vijana ambao walishindwa kufanya vema katika masomo yao ya kidato cha nne ama kuishia darasa la saba kutokana na changamoto kadhaa walizokuwa wakizipitia.
“Nimetaarifiwa kuwa hawa wanafunzi wanapojiunga katika chuo hiki wanalipia Shilingi 50,000 tu kwa jili ya gharama za vifaa na fedha nyingine zinagharamiwa na chuo hadi wanapohitimi, hivyo niupongeze uongozi wa Chuo kwa jitihada hizo za kuwainia kielimu na kutimiza ndoto za vijana ambazo tayari zilikuwa zimepotea.
“Kulingana na jitihada ambazo zimeoneshwa na Furahika, wahitimu msikiangushe chuo hiki mkawe mabalozi wazuri huko mwendako na mkajiendeleze kielimu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuajiriwa na kujiari”amesema
Mbassa kwa niaba ya Mwenyekiti CCM wa Wilaya Ilala, ametoa wito kwa wazazi kuwa mabalozi wazuri kwa wazazi wengine ili walete watoto wao wapate mafunzo ya kozi zitakazowasaidia kupambana na maisha na kuwatoa katika lindi la umasikini na kuzagaa mtaani bila kazi maalumu.
Pia amesema kutokana na changamoto zilizopo chuoni hapo ambazo ziliwasilishwa na msoma risala, amezibeba na atazipeleka katika vikao vyao na Chama na Serikali ili kuzifanyia kazi ili kuleta tija stahiki katika chuo hicho ambapo kimekuwa mkombozi kwa vijana wengi waliopoteza matumaini baada ya kufanya vibaya katika masomo yao ya kidato cha nne ama darasa la saba kwa kupata alama hafifu na kushindwa kuendelea na masomo.
Naye, Marton Mkuu, Happyness Sanga kutoka Wanyama Hoteli ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika mahafali hayo amesema kwamba wako tayari kutoa nafasi tisa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na wakifanya vizuri , wote watapatiwa ajira ya moja kwa moja.
“Tuna matawi mawili ya hoteli, moja ikiwa Sinza wilayani Ubungo ya pili ipo Kariakoo hivyo kwa wahitimu hawa tunachukua tisa kama watafanya vizuri, wote watapatiwa ajira ya moja kwa moja ingawa wanatakiwa kifikia vigezo ikiwamo kuwa na utii, nidhamu na bidii katika kazi, atakayeshindwa tutamrudisha hapa kwa Msuya,” amesema.
Naye Belinda Malisa ambaye ni msoma risala akiwawakilisha watihimu, amesema kuwa Chuo hicho kimekuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na kutokana na mwaka huu wa masomo wanafunzi wengi kupokelewa kwa ajili ya kujiunga na kozi mbalimbali chuoni hapo.
“Pia chuo hiki kinaupungufu wa vifaa vya Tehama , kwa wanafunzi wanaochukua masomo yanayohusu teknelojia hiyo, hivyo ombi letu kwa mgeni rasmi kututafutia wafadhiri wa kuziba changamoto hizo na nyinginezo zilizopo hapa chuoni,” amesema.