Pic DSC02292-Ofisa Ugavi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Jiji la Mwanza, Shamsa Adam,akifundisha washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa mradi wa kupuguza umasikini mada ya manunuzi leo.
Mhasibu wa TASAF Jiji la Mwanza,Zawadi Hussein, leo akiwafundisha wajumbe wa serikali za mitaa na kamati ya usimamizi wa mradi wa kupuguza umasikini wa mitaa ya Shamaliwa A na Kilimo B,namna ya kuingiza na kutoa vifaa leja.
Diwani wa Igoma (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii,Uchumi, Elimu,Afya na Mazingira Jiji la Mwanza,Mussa Ngollo, leo akifunga mafunzo yaliyoshirikisha wajumbe na kamati ya usimamizi wa mradi wa kupunguza umasikini kutoka mitaa ya Shamliwa A na Kilimo B.
Washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa mradi wa kupunguza umasikini kutoka mitaa ya Shamaliwa A na Kilimo B, leo wakimsikiliza Diwani wa Igoma (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii,Uchumi, Elimu,Afya na Mazingira Jiji la Mwanza,Mussa Ngollo,wakati akifunga mafunzo hayo.
……..
NA BALTAZAR MASHAKA,NYAMAGANA
WASIMAMIZI wa Mradi wa Kupunguza Umasikini wilayani Nyamagana jijini Mwanza,wametakiwa kuutumia uelewa walioupata kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa kijamii.
Rai hiyo imetolewa leo na Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)Jiji,Peter Ngagani,wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa wajumbe na kamati ya jamii usimamizi wa mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula,madarasa na matundu ya vyoo katika shule ya Shamaliwa sekondari,kutoka mitaa ya Kilimo B na Shamaliwa A,Kata ya Igoma.
“Serikali ilianza na bweni leo imekuja na miradi miwili, tukatumie uelewa tuliopata kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa kijamii katika sekta ya elimu na tusipoze, tukipoza tutalazimika kutumia nguvu kubwa kuishawishi jamii kuchangia nguvu zao,”amesema Ngagani na kuongeza wasipopata mingine ya jengo la utawala na nyumba mwalimu,kikwazo kitakuwa ni hao wasimamizi.
Ngagani amesema baada ya mafunzo hayo wameingia kazini na jamii inapaswa kushirikishwa kile wanachokwenda kukisimamia ambapo tyari serikali imeshatoa fedha za mradi huo utakaotumika kuwaandaa watoto kielimu,asitokee mtu wa kukwamisha au kuachia wengine jukumu la kusimamia.
Ameeleza kuwa mradi huo ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii kwa kuwaandaa watoto kielimu na kijamii, utapunguza changamoto ya ajira na baadhi vijana watapata ajira za kitaaluma na zisizo za kitaaluma,hivyo usiishie njiani kwani utakuwa na madhara makubwa kwa jamii.
Ngagani amesema Serikali kupitia TASAF inatekeleza miradi ya elimu,afya na miundombinu ya barabara kuwawezesha wananchi kupata huduma za msingi karibu,ambayo inatumia dhana ya ushirikishaji wa jamii kuchangia asilimia 10 na kuwasistiza wajumbe na kamati ya usimamizi wakawaeleze wananchi madhara ya watoto kukosa elimu.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo wa TASAF Jiji,Kata ya Igoma haikuwa na shule ya kidato cha sita hivyo wameipa kipaumbele cha kujenga shule ya mfano itakayokuwa darasa kwa wengine kujifunza kwa sababu miradi yote iko eneo moja.
Pia,mafunzo yataiwezesha kamati kusimamia miradi ya kijamii na katika kutekeleza mradi huo ushiriki wa nguvu kazi ya jamii ni asilimia 10 ambao utasaidia kuchimba msingi,kusaidia mafundi,kusomba maji na kusogeza mawe,TASAF asilimia 90.
Hivyo,jamii ikishindwa kuchangia mradi ni changamoto,itambue mradi ni wao wala si mali ya TASAF ambayo inawezesha kukamilisha tu.
Ofisa Ufuatiliaji TASAF Makao Makuu,Samson Kagwe amesema mradi huo wa Kupunguza Umasikini Awamu ya Nne utaimarisha dhana ya ushiriki wa jamii katika mchakato wa maendeleo na kuhakikisha maisha bora ya kutokomeza umasikini mkoani humu na nchi hatimaye kujiletea maendeleo yatakayowanufaisha Watanzania wote.
Akifunga mafunzo ya Wajumbe wa Serikali za Mitaa na Kamati ya Usimamizi wa mradi,leo Diwani wa Igoma, Mussa Ngollo amewataka watunza stoo na vifaa vya mradi wazingatiye uadilifu na uzalendo katika usimamizi na utoaji wa vifaa kuepuka ubadhirifu unaoweza kuisababishia serikali hasara hasa vifaa vikipotea italeta sifa mbaya.
“Tuonyeshe uzalendo na uadilifu katika mradi huu ili kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ametukumbuka kwa kutoa fedha kuwezesha watoto wetu wasisafiri umbali mrefu wakitafuta huduma ya elimu,”amesema.
Ngollo amesema katika kuunga mkono jitihada za serikali kuwaletea maendeleo wananchi wataendelea kushirikiana nayo kuhakikisha malengo inayotarajia kwa wananchi yanafikiwa kwa kutatua changamoto za elimu,afya,maji na miundombinu ya barabara.