Makongamano ya wadau yanayoendelea nchini kuhusu marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 yanalenga kukusanya maoni yatakayosaidia kutengeneza Sera ya Mambo ya Nje Bora itakayoongoza ushirikiano wenye tija baina ya Tanzania na nchi nyingine, mashirika ya kikanda na kimataifa.
Hayo yamesemwa leo tarehe 10 Februari 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu – Zamzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir wakati akisoma hotuba ya ufunguzi ya Kongamano la nne la wadau lililofanyika kisiwani Pemba.
Makongamano hayo yanayoratibiwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Rais-Zanzibar na Taasisi ya Uongozi yametajwa kuwa ni kielelezo cha utawala bora ambao unahimiza ushirikishwaji wa wananchi katika utengenezaji wa Sera za Taifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) amesisitiza umuhimu wa wananchi walioshiriki kongamano hilo kutoa maoni yao kwa uhuru bila woga.
Alisema maoni yao yatasaidia kutengeneza Sera ya Mambo ya Nje madhubuti itakayoifanya Tanzania kutetea maslahi yake katika majukwaa ya Kimataifa na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika dunia ya sasa.
Alisema mijadala yao ya kurekebisha Sera ya Mambo ya Nje itatoa mwelekeo wa kuboresha maeneo mapya yanayopendekezwa ambayo ni pamoja na masuala ya uchumi wa Buluu, diaspora, mabadiliko ya tabianchi, kubidhaisha Lugha ya Kiswahili na kulinda mila na desturi za Tanzania.
Balozi Mbarouk alimsifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Sera ya Mambo ya Nje amabo umesaidia kuongezeka kwa ajira za Watanzania katika mashirika ya kikanda na Kimataifa, masoko ya bidhaa za Tanzania Nje ya nchi, misaada na mikopo ya Maendeleo, uenyeji wa taasisi za kimataifa nchini na ujenzi wa miradi ya Maendeleo katika sekta mbalimbali za miundombinu, nishati, kilimo, elimu na afya.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa makongamano yaliyofanyika Arusha, Dar Es Salaam na Unguja limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kusini-Pemba, Mhe. Matar Zahor Masoud; Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Bw. Salehe Juma Mussa, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shwaibu Mussa; baadhi ya Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi; wawakilishi wa vyama vya siasa; asasi za kiraia; jumuiya za kidini na wananchi kwa ujumla.