Muonekano wa mtambo wa kuzalisha Umeme wa gesi asilia wa Megawati 20 unaotumia injini ya ndege aina ya Boing 747 ulitengenezwa nchini Marekani kwa ajili ya kutatua changamoto ya Umeme Lindi na Mtwara.
Baadhi ya wananchi na wa kazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakiangalia mtambobwa Megawati 20 uliowasili mkoani Mtwara ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais kutatua changamoto za Umeme mikoa ya Kusini
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza wakati wa hafla ya kupokea mtambo wa kuzalisha Umeme wa gesi asilia Megawati 20 kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara.
……………………..
*Mtambo wa Megawati 20 wawasili mkoani Mtwara
*Wabunge wapongeza
MTWARA
Serikali imeendelea kutekeleza ahadi ya kupeleka umeme wa uhakika katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameongoza mapokezi ya mtambo wa megawati 20 utakaozalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia.
Mtambo huo aina ya TM16 wenye mfano wa injini ya ndege ya Boeing 747 utafungwa katika Kijiji cha Hiari, Wilaya ya Mtwara Vijijini ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa changamoto ya upatikanaji umeme kwenye mikoa hiyo inatatuliwa.
Akipokea mtambo huo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, amesema kuwa mtambo huo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme kwenye Mkoa wa Lindi na Mtwara.
“ Mhe. Rais alitoa maelekezo kwa Wizara ya Nishati, kufanya kila jitihada ili changamoto ya umeme kwenye mikoa hiyo itatuliwe kwa haraka, tunashukuru leo tumeweza kutimiza ahadi hiyo kwani mtambo huu ni miongoni mwa mitambo ya kisasa kabisa ya umeme iliyowahi kuletwa nchini ambayo inatoa uhakika wa kuzalisha umeme kwa kipindi kirefu.” Amesema Mha.Mramba
Aidha, Mhandisi Mramba ameongeza kuwa, maelekezo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuhusu kuepeleka umeme wa gridi kwenye mikoa hiyo yameshaanza kutekelezwa ambapo kabla ya mwezi wa sita mwakani umeme wa Gridi ya Taifa utakuwa umefika kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kuhusu maelekezo aliyoyatoa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ya kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo inayozalisha gesi kwa wingi wananufaika na uwepo wa nishati hiyo, amesema tayari wameanza kuboreshewa huduma mbalimbali ikiwemo kuwajengea kituo cha Polisi, ununuzi wa boti ya kisasa kwa ajili ya usafiri wa wananchi eneo la Songosongo mkoani Lindi na ujenzi wa kituo cha afya eneo la Madimba mkoani Mtwara..
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed alisema kuwa, wananchi wa Mtwara wamepokea kwa furaha mtambo huo ambao utafungua fursa za uwekezaji kwa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika kwani takriban asilimia 80 ya matumizi ya umeme mkoani humo yanatumika kwenye sekta ya biashara.
“ Tunamshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. Samia kwa kutimiza ahadi yake na na mapenzi ya dhati aliyoyaonyesha kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara na kufanya mikoa hii kupata umeme wa uhakika ambao utainua sekta ya uchumi kwa ujumla.” Amesema Kanali Ahmed
kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda ameishukuru Serikali kupitia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko kwa kusikiliza kilio cha wabunge wa mikoa juu ya changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuipongeza Wizara ya Nishati kwa hatua kubwa inazochukua kuhakikisha sekta ya umeme inaimarika.