Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Ridhiwan Kikwete akizungumza katika mkutano huo mkoani Arusha.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada mbalimbali mkoani Arusha.
……
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Ridhiwan Kikwete amewataka Wakuu wa maswala ya Tehama kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuweza kudhibiti wizi wa mitandaoni kwani umeshamiri kwa kiwango kikubwa na watu wanaendelea kutapeliwa kila siku.
Ameyasema hayo mkoani Arusha leo wakati akifunga kikao kazi cha 4 cha wadau wa serikali mtandao kilichowashirikisha zaidi ya wadau 1,300.
Kikwete amesema kuwa, hivi sasa kumekuwepo na wimbi kubwa la wizi unaofanyika kwenye mitandao jambo ambalo linahitajika kudhibitiwa kwa haraka.
“Ni vizuri mitandao hii ikatumika kwa faida ya wananchi ikiwemo kuweka mipango madhubuti na mikakati ya kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa kutosha katika matumizi ya mitandao na hatimaye malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa. “amesema Kikwete.
Aidha amewataka pia kuhakikisha wanajenga misingi mizuri katika utekelezaji wa serikali mtandao ikiwa ni pamoja na kuwa na mshikamano na kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu hayo.
Hata hivyo alilitaka taasisi za umma ambazo hazijaingia kwenye mfumo huo kufanya hivyo mara moja ili kuwezesha upatikanaji wa mawasiliano kwa pamoja na kuwafikia wananchi kwa haraka.
“Wakuu wote wa taasisi nawaomba mhakikishe mnawapa nafasi za kutosha wakuu wa Tehama katika kuhakikisha wanashiriki katika vikao mbalimbali kwa lengo la kuimarika na kujifunza zaidi kwani teknolojia inabadilika kila siku na ni lazima tuendane nayo.”amesema Kikwete
Aidha ameongeza kuwa ,katika maazimio hayo kumi waliyofikia ni vizuri wakahakikisha yote wanayafanyia kazi ili wakikutana tena kwa kikao kingine mwakani waelezee walipofikia na maboresho waliyoyafanya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa serikali mtandao ,Benedict Nbomba amesema kuwa,kwa siku tatu wameweza kujadili maswala mbalimbali ikiwemo kuweka maazimio kumi ambayo kila mmoja ataenda kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha taasisi zao.
Amesema miongoni mwa maazimio waliyoweka ni pamoja na kuandaa tuzo kwa taasisi zitakazofanya vizuri na zile ambazo hazitafanya vizuri pia zitatajwa ili kuendelea kuwepo kwa ushindani zaidi katika Taasisi hizo.
Aidha amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na taasisi hizo katika kubuni na kutoa huduma bora kwa wananchi lengo likiwa ni kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo hapo awali.
“Tutahakikisha mamlaka inasaidia taasisi zote kufanya kazi kwa weledi na kwa mikakati iliyowekwa ili kufikia serikali ya kidigitali ambalo ndilo lengo kuu.
Naye mwikilishi wa washiriki akizungumza kaa niaba ya washiriki amesema kuwa,kikao hicho kimeweza kuwa cha mafanikio makubwa baada ya kuweza kujadili changamoto na namna ya kuweza kuboresha ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha amesema kuwa wameweza kujadili kuhusu usalama wa mitandaoni ambao kwa pamoja wameweka mikakati ya namna ya kulifanyia kazi swala hilo kwa kushirikiana taasisi mbalimbali.
“Pia tumeweza kuweka maazimio kwa taasisi zote ambazo hazijajiunga na mfumo huo kuhakikisha wanajiunga haraka ili kwa pamoja tuweze kuwa na mfumo mmoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.