Na Issa Mwadangala
Wazazi na walezi wametakiwa kutofumbia macho na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Wito huo ulitolewa Februari 08, 2024 na Mkaguzi kata wa Kata ya Ruanda Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Happy Lumbe alipofanya mkutano wa kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake wa kata ya Ruanda Wilayani Mbozi.
Alisema ukatili wa kijinsia kwa watoto unatakiwa kupingwa na kila mzazi au mlezi anapaswa kuwajibika kumlinda mtoto wa mwenzie kama anavyomlinda mtoto wake dhidi ya vitendo hivyo.
Sambamba na hayo alisisitiza kuishi katika mazingira salama ya kujikinga na magonjwa milipuko kama Kipindupindu ambacho kwa kiasia kikubwa kinatokana na uchafu wa mazingira. Amefafanua kwamba usafi ni pamoja na kuwa na vyoo safi.
Aidha alisema malezi bora ya watoto ni kuhakikisha watoto hao wanapata elimu, hivyo amewataka wazazi kuwapeleka watoto shuleni kwa wakati ili wapate haki yao ya msingi.
Kwa upande wa wanawake wa kata hiyo wamepongeza juhudi za Jeshi la Polisi kusogeza huduma hizo katika ngazi ya kata jambo ambalo linasaidia kupata elimu kwa kiasi kikubwa tofauti na hapo nyuma.