Na. James Mwanamyoto-OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Mfumo wa Taifa wa Manunuzi wa Kielektroniki (NeST) hauna mbadala katika kufanya mchakato wa manunuzi kwenye ngazi ya halmashauri.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo jijini Dodoma, wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba iliyoibuka kinara nchini katika matumizi ya Mfumo wa Taifa wa Manunuzi wa Kielektroniki (NeST).
Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa halmashauri na taasisi zinazolegalega kutumia mfumo wa NeST kuanza kuutumia kwani hakuna mbadala, hivyo watendaji wote walio chini ya OR-TAMISEMI wanapaswa kujifunza na kuutumia kikamilifu.
Ameongeza kuwa, kitendo cha Halmashauri ya Kwimba kupata tuzo ni somo kwamba hakuna mjadala kuhusu matumizi wa mfumo wa NeST kwa halmashauri zote zilizopo pembezoni ambazo husingizia changamoto ya mtandao.
“Halmashauri ya Kwimba ipo mbali lakini imefanikiwa katika matumizi ya mfumo wa NeST hivyo sijui ni kwanini Halmashauri zilizopo mijini zinashindwa kuutumia mfumo huu wakati wana umeme na mtatandao wa uhakika,” Waziri Mchengerwa amehoji.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amemtaka Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuzielekeza Halmashauri zote kuhusu matumizi ya mfumo wa NeST.
Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa watendaji wote waliochini ya OR-TAMISEMI ambao wanakabiliana na changamoto katika matumizi ya mfumo wa NeST, kuwasiliana na PPRA kupitia namba ya simu 0736 494 948 au kwa barua pepe: [email protected] au kuwasilianao kupitia live chart iliyo katika mfumo wa NeST.
Mfumo wa Taifa wa Manunuzi wa Kielektroniki (National e-Procument System of Tanzania-NeST) unasimamiwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma(PPRA).