Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw.Mavere Tukai wakati alipotembelea banda la taasisi hiyo katika Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Tarehe 09 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati alipotembelea banda la taasisi hiyo katika Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Tarehe 09 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na viongozi mbalimbali wakiwasili katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo tarehe 09 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwaongoza kuimba wimbo wa Taifa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Tarehe 09 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Tarehe 09 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi tuzo Muuguzi Kiongozi wa Kwanza wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Bi. Salome Kassanga wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar. Tarehe 09 Februari 2024.
…………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema jitihada inahitajika katika kutoa elimu ya magonjwa yasioambukiza pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha, mazoezi na kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya moyo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport – Unguja, Zanzibar.
Amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa moyo ni muhimu wananchi kufuata njia za kujikinga zaidi ikiwemo kuacha ulevi uliyopindukia, uvutaji sigara, tabia bwete pamoja na uzito uliyopindukia.
Ametoa rai kwa watalaamu wa afya, wasomi, vyombo vya habari pamoja na watunga sera kushiriki katika utoaji elimu kuhusu masuala ya afya.Aidha Makamu wa Rais amesema tafiti zinapaswa kufanyika kwa kina ili kubaini visababishi zaidi vya magonjwa ya moyo kwa kupata taarifa zaidi juu ya taratibu za kijamii na tabia za kiutamaduni katika mambo mbalimbali yaliyozoeleka kufanyika barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo kama vile kuimarisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kufanya tafiti za afya za kimkakati ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wananchi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa adimu.
Amesema Taasisi ya Moyo ya jakaya Kikwete imeendelea kuimarika ambapo kwa sasa inafanya upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 800 kwa mwaka ikiwemo upausaji wa kufungua kifua (upasuaji mkubwa) ukilinganisha na wagonjwa 200 wakati ikianzishwa. Amesema zaidi ya wagonjwa laki mbili hutibiwa kwa mwaka huku zaidi ya 2400 wakitoa mataifa mengine.
Ameongeza kwamba serikali imeweza kuokoa zaidi ya bilioni 63 kila mwaka za matibabu ya wagonjwa wa moyo kutokana na kuimarishwa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Vilevile Makamu wa Rais amesema serikali itaongeza uwekezaji katika huduma za magonjwa ya moyo na kuandaa mipango ya awali, ubunifu, tafiti , mafunzo, ushirikiano, udhibiti na utoaji tiba wa magonjwa ya moyo nchini.
Mkutano huo wa siku mbili uliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete unawakutanisha Madaktari Bingwa, wataalam na wadau wa afya, wauguzi na watunga sera kutoka mataifa zaidi ya 40 duniani kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusu magonjwa ya moyo duniani.Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais09 Februari 2024Zanzibar.