NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi amesema Shule ya Sekondari ya Hagati wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma inatarajia kuanza kupokea rasmi wanafunzi wa kidato cha tano na sita Julai 2024.
Mhe Ndejembi ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini, Mhe Benaya Kapinga aliyehoji ni lini Shule hiyo itapandishwa hadhi kuwa ya kidato cha tano na sita.
“ Serikali ilipeleka fedha kiasi cha Sh Milioni 128 kwa ajili ya ujenzi wa bweni, ujenzi huo tayari umeshakamilika na taratibu za usajili wa kidato cha tano unaendelea na tayari Halmashauri imeshaomba kibali cha kupandisha hadhi ya kuwa kidato cha tano na sita. Hivyo shule hiyo inatarajia kuanza rasmi kwa kidato cha tano na sita Julai mwaka huu,” Amesema Mhe Ndejembi.