Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema serikali inakusudia kuwekeza nguvu nyingi katika ujenzi na ukarabati wa barabara kwa kutumia teknolojia mbadala ya ECO Road.
Teknolojia hiyo itatumika kwenye barabara zilizochini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ikilenga katika kuongeza ufanisi wa gharama na muda wa utekelezaji wa miradi na utunzaji wa mazingira.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya TARURA kuhusu marekebisho ya miundombinu ya barabara na tathimini ya uharibifu wa miundombinu ya barabara katika kipindi cha Julai 2023 hadi Januari 2024 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Amesema dhamira ya kutumia teknolojia ya ECO Road ni kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za wilaya ili angalau asilimia 85 ya barabara hizo iweze kupitika misimu yote ifikapo mwaka 2025.
Akizungumzia tathimini ya uharibifu wa miundombinu nchini, Waziri Mchengerwa amesema TARURA inahitaji shilingi bilioni 131 kurekebisha uharibifu wa miundombinu uliotokea katika mikoa yote 26 katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni 2023, hadi mwezi January 2024.
Wakichangia taarifa hiyo baadhi ya wajumbe wa kamati akiwemo Mbunge wa Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi wameshauri ujenzi wa mitaro mikubwa kandokando mwa barabara zinazojengwa na TARURA na akitolea mfano wa baadhi ya barabara zenye mitaro mikubwa zilizojengwa na TARURA katika jimbo lake zilivyosaidia kudhibiti mafuriko yaliyokuwa yakitokea katika maeneo hayo kila mwaka.
Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Denis Londo ameipongeza TARURA kwa kazi kubwa wanayoifanya na kushauri juu ya uanzishwaji wa jumuiya za watumiaji barabara na kuhimiza kuzijengeaa uwezo ili zisaidie katika kusimamia miundombinu ya barabara.
Mpaka sasa serikali kupitia TARURA inaendelea na majaribio ya ujenzi wa barabara kwa kutumia teknolojia mbili tofauti ambapo inajenga barabara ya Sawala- Mkonge- Iyegeya hadi Lulanda mkoani Iringa yenye kilometa 10.4 ambayo kwa teknolojia ya ECO Road na ujenzi wake umefikia asilimia 55, na inajenga barabara ya kilometa tano kutokea eneo la Itilima Oli hadi Ikindilo Mkoani Simiyu kwa teknolojia ya Ecozyem.