Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi moyo ya Jakaya Kikwete Dkt.Peter Kisenge akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo unaotarajia kufanyika Golden tulip fubuari 09 mwaka huu.
Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Asha Ressa Izina akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo unaotarajia kufanyika Golden tulip fubuari 09 mwaka huu .
Mratibu wa mafunzo ambae ni Mkuu wa Kitengo na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ya watoto Dkt. Godwin G. Sharaw akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo unaotarajia kufanyika Golden tulip fubuari 09 mwaka huu.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika mafunzo ya vitendo ya kuunganisha mishipa ya damu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete huko Verde Mtoni Zanzibar (PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR)
……
Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kufanya mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo katika ukumbi wa Golden tulip Febuari 09 mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya mkutano huo huko Hotel ya Verde Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt.Peter Kisenge amesema lengo la mkutano huo ni kuwawezesha madaktari wazawa wa hospitali zote kuanzia ngazi za chini hadi Taifa kubadilishana mawazo na uzowefu kutoka kwa washiriki wa nchi mbalimbali.
Aidha alisema mkutano huo utawawezesha watu wa nchi za Afrika kuilewa taasisi hiyo na huduma zinazotolewa jambo ambalo litapelekea kupunguza gharama za kujitibu nje ya nchi.
Dkt.Peter alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza vifaa na rasilimali watu katika taasisi hiyo jambo ambalo limepelekea kuwa kimbilio la wagonjwa wa moyo kutoka nchi mbalimbali.
Alisema kutokana na mabadiliko ya teknolojia mkutano huo unaenda sambamba na mafunzo maalum ya vitendo kwa madaktari wa upasuaji juu ya mambo mbalimbali ikiwemo uvunaji wa mishipa ya moyo, na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa mahututi yaliyoanzia Febuari 08 hadi 10 katika Hoteli ya Verde Mkoa wa Mjini Zanzibar.
Alifahamisha kuwa wawakilishi zaidi ya 500 wazawa na 40 kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo ikiwemo madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
Hata hivyo aliwakumbusha waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huo ili kujikinga pamoja na kuokoa fedha nyingi za Serikali zinazotumika kusafirisha wagonjwa hao.
Mapema dkt. Peter alifahamisha kuwa mkutano huo wenye kauli mbiu “Maendeleo ya matibabu ya moyo katika nchi za Afrika“ utafunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango na kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe, Dkt.Hussein Ali Mwinyi Febuari 10 mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ya watoto Godwin G. Sharaw amesema katika mafunzo hayo watahakikisha wanagusa kila eneo linalohusiana na magonjwa hayo ili kuhakikisha lengo linafikiwa.
Alisema madaktari hao watapata kujifunza changamoto za matibabu ya moyo, maendeleo mapya juu ya ugonjwa huo, upasuaji kwa kutumia tundu dogo, kuziba mishipa pamoja na kuunganisha mishipa ya damu.
Nae Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Asha Ressa Izina amesema ili kuhakikisha teknolojia zinatumika kwa usahihi ni lazima kuwa na watu wenye uwezo wa kuzitumia ili kuhakiksha huduma bora zinatolewa kwa walengwa.
Hivyo mkutano huo utakaozungumzia huduma za moyo katika nchi za Afrika sambamba na mafunzo mbalimbali yatakayowasilishwa na madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi yatawasaidia madaktari kutoa huduma bora na kuijengea uelewa jamii kujua viashiria vya ugonjwa huo.
Itakumbuka kuwa takribani watoto elfu 16 huzaliwa na magonjwa ya moyo kati yao mia nne wanahitaji upasuaji ndani ya mwaka mmoja mara tu baada ya kuzaliwa.