Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo 

Na Albano Midelo,Mbinga 

MKUU wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mheshimiwa Aziza Mangosongo ametoa rai kwa wakulima kulima mazao mengine ya biashara  badala ya kutegemea  zao la Kahawa peke yake.

Mangosongo ametoa rai hiyo ofisini kwake mjini Mbinga, kwenye mkutano na wakulima pamoja na wadau wa zao la parachichi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbinga amewasisitizia   wakulima wa kahawa kulima mazao mchanganyiko  ili  kuwawezesha kupanua wigo wa mapato yao.

“Bei ya kahawa inaposhuka, zao mbadala kama parachichi linaweza kuwa msaada kwako na hivyo kukufanya usitetereke kiuchumi,” alisisitiza Mangosongo na  kuongeza kuwa zao la parachichi licha ya kuwa chanzo cha mapato ni rafiki wa mazingira’’,alisema Mangosongo.

 Mtaalam wa kilimo katika zao la Parachichin Frank Nyoni  amesema kitaalamu parachichi  ni tunda lenye virutubisho muhimu sana vinavyohitajika katika mwili wa binadamu na linaongeza kipato kwa familia na Taifa.

Amelitaja soko la parachichi hivi sasa limekuwa sana kutokana na  kupeleka zao hilo nje ya nchi Pamoja na usindikaji  wa bidhaa zinazotokana na  parachichi ambapo hivi sasa bei ya tunda moja la parachichi sokoni inaanzia shilingi 500 hadi 1500

Nchini Tanzania parachichi hulimwa zaidi katika mikoa ya Iringa, Ruvuma,Njombe,Mbeya,Katavi,Rukwa,Morogoro na Kilimanjaro.