Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe.Abdulaziz M.Abood amekabidhi Gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) Hospitali ya Wilaya ya Morogoro Mjini litakalosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Ambulance hiyo imetolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni matokeo ya maombi ya Mhe. Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kwa ajili ya Hospitali hiyo.
Katika makabidhiano hayo, viongozi mbalimbali wa chama Serikali walishiriki ikiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Ally Machela, wakuu wa Idala ya Afya, Uchumi na Manunuzi.
Akizungumza katika Halfa hiyo Mhe. Abood amempongeza na kumshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Samia kwa gari la kubebea wagonjwa alilolitoa kwa ajili ya Wananchi wa Morogoro Mjini ambao awali walikuwa wanapata changamoto ya usafiri wakipata rufaa ya kutoka kwenye vituo vya afya kwenda Hospital ya Rufaa ya Morogoro.
“Namshukutu sana Mhe. Rais kwani amekuwa msikivu kila ninapomuomba kutatua changamoto za wana Morogoro Mjini, ametoa fedha nyingi katika ujenzi wa Miradi ya Afya, Ununuzi wa Vifaa na Vifaa tiba vya kisasa na huduma za Dawa kwa ajili ya kutolea huduma katika Jimbo la Morogoro Mjini.” Alisema Abood
Pia Mhe. mbunge amewapongeza Madaktari na wahudumu wote wa afya katika Hospitali ya Wilaya, Divisioni ya Afya na maendeleo ya Jamii sambamba na Viongozi wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi wa manispaa kwa Kazi nzuri wanazozifanya kwenye idara hiyo.