Mratibu wa TASAF Jiji la Mwanza, Peter Ngagani , akiwasilisha mada ya majukumu ya Kamati za Jamii za Usimamizi wa Mradi (CMC) na Wajumbe Serikali za Mitaa (VC) wakati wa mafunzo yaliyofanyika, leo Igoma wilayani Nyamagana.
Diwani wa Igoma (CCM) Mussa Ngollo, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, leo akifungua mafunzo kwa Kamati za Jamii za Usimamizi wa Mradi (CMC) na Wajumbe Serikali za Mitaa (VC) Kata ya Igoma wilayani humo.
Ofisa Ufuatiliaji wa TASAF Jiji la Mwanza, Samson Kagwe,akifafanua jambo kwa Kamati ya Jamii ya Usimamizi wa Mradi na Wajumbe wa Serikali za Mitaa kuhusu Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umasikini (TPRP IV).
Kamati ya Jamii ya Usimamizi wa Mradi (CMC) na Wajumbe wa Serikali za Mitaa (VC),leo wakiwa katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wa mchakato wa mradi wa Kupunguza Umasikini unaotekelezwa Kata ya Igoma, wilayani Nyamagana.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkapa, Kata ya Igoma ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa miradi ya jamii, akieleleza jambo wakati wa mafunzo hayo leo. (Picha zote na Baltazar Mashaka )
……….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SERIKALI wilayani Nyamagana imeeleza kuwa Jiji la Mwanza linatarajia kupokea zaidi ya sh.bilioni 1.2 za miradi 15 ya Kupunguza Umasikini Awamu ya Nne (TPRP IV) katika sekta za elimu,afya na miundombinu barabara.
Hayo yalielezwa leo na Diwani wa Igoma (CCM) Mussa Ngollo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilangi wakati akifungua mafunzo kwa Kamati ya Jamii (CMC) ya Usimamizi wa Mradi na Wajumbe wa Serikali za Mitaa (VC).
Amesema Jiji linatarajia kupokea fedha sh. bilioni 1.24 kutekeleza miradi 15 kwa mwaka wa pili kwa kuzingatia muundo wa mradi,mitatu (3) ya ajira za muda kwa walengwa,10 ya uendelezaji miundombinu katika jamii na miwili ya kuongeza kipato cha kaya.
Ngollo amesema kwa mwaka wa kwanza Jiji la Mwanza lilishapokea jumla ya miradi 10, awamu ya kwanza miradi mitano katika kata za Igoma na Mahina,awamu ya pili pia mitano ambayo inaanza kutekeleza katika kata hizo.
Amefafanua miradi hiyo ilibuniwa kupunguza athari za umasikini,ikilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kuchumi na kijamii katika ngazi za jamii zilizo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kupitia mradi huu jamii zitatekeleza miradi ya elimu,afya na miundombinu ya barabara yenye upungufu wa huduma hizo.
Aidha,miradi hiyo itatekelezwa katika ngazi ya kaya za walengwa wanaohudumiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kuongeza upatikanaji wa chakula,kukuza uchumi wa kaya na kupata huduma za msingi za kijamii.
Ngollo amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, Oktoba 2021 jijini Dodoma alielekeza matumizi ya fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),akieleza kwa kina umuhimu wa kuweka mkazo zaidi kutekeleza miradi ya elimu, afya, maji na kuondoa umasikini wa kipato ili kuziwezesha kaya masikini kutoka katika utegemezi.
Aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa,mkakati wa dunia nzima ni kunusuru jamii masikini na watu wa makundi maalum,umakini mkubwa wa kitaalamu unahitajika katika mradi huu kuhakikisha miradi ya kijamii inayotekelezwa inaonesha thamani ya fedha na niwaase kuzingatia maelekeo yatakayotolewa hatimaye kufikisha ujumbe sahihi katika ngazi mbalimbali.
Kwa mujibu wa diwani huyo utekelezaji wa miradi ya TPRP jijini Mwanza utaendeleza na kuimarisha dhana ya uwazi, ukweli,ushirikishwaji na uwajibikaji kwa kuwa ina dhana hiyo, viongozi wawajibike kuhakikisha jamii iwajibika kwa kuchangia matumizi ya nguvu kazi inayohitajika kulingana na bajeti.
Pia,katika kumuunga mkono Rais Dk.Samia ambaye amesimama kidete kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za jamii kwani upatikanaji wake unaambatana na uzalishaji unapunguza umasikini kwa haraka na hivyo viongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri wafuatilie miradi hiyo itakayowezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati na wasimamizi wa mpango wakafanye kazi kwa weledi.
Naye Ofisa Ufuatiliaji wa TASAF Jiji,Samson Kagwe ameeleza miradi ya mwaka wa pili Jiji linatarajia kupokea sh.bilioni 1.24,limeshapokea sh.milioni 775 za miradi husika ambapo sh.milioni 401 za ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la Zahanati ya Mahina na bweni la Shamaliwa sekondari,ujenzi wa Bwalo la chakula, madarasa 3 na matundu 6 ya vyoo yatakayojengwa Shamaliwa sekondari na jengo la upasuaji Mahina zahanati sh. milioni 374.
Amesema Serikali kupitia TASAF imeendelea kutekeleza miradi ya wananchi wapate huduma za msingi katika sekta za elimu,afya na miundombinu miradi ambayo inatumia dhana ya ushirikishwaji wa jamii kabla kamati za usimamizi zitapata mafunzo ya siku tatuzifahamu michakato ya miradi.
“Mradi huo wa Kupunguza Umasikini Awamu ya Nne utawezesha kuimarisha dhana ya ushiriki wa jamii katika mchakato wa maendeleo na hivyo kuhakikisha misha bora ya kutokomeza umasikini mkoani humu na nchi na kujiletea maendeleo yatakayowanufaisha Watanzania wote,”amesema Kagwe.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Jiji, Peter Ngagani ameeleza Kata ya Igoma haikuwa na shule ya kidato cha sita hivyo imekuwa kipaumbele cha kujenga shule ya mfano itakayokuwa darasa la watu wengine kujifunza kwa kuwa miradi yote iko eneo moja.
Amesema mafunzo yanayotolewa yataiwezesha kamati kusimamia miradi ya kijamii pia katika kutekeleza mradi huo ushiriki wa nguvu kazi ya jamii ni asilimia 10,utasaidia kuchimba msingi,kusaidia mafundi,kusomba maji na mawe.
Hivyo,jamii inaposhindwa kuchangia mradi ni changamoto,itambue mradi ni wao na si mali ya TASAF ambayo inawezesha kukamilisha tu,hivyo wachangie ikamilike ndani ya miezi mitatu na kuitunza.