Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba, Bw. Ahmad Abdalla kulia na Mkurugenzi Benki ya PBZ, Dkt. Muhsin Masoud wakitiliana saini makubaliano kwa ajili ya kufanya uwezeshaji wa kuwakopesha watanzania nyumba zenye ubora kwa gharama nafauu kwa mkopo wa muda wa miaka 25.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba, Bw. Ahmad Abdalla kulia na Mkurugenzi Benki ya PBZ, Dkt. Muhsin Masoud wakionesha mkataba mara baada ya kutiliana saini makubaliano kwa ajili ya kufanya uwezeshaji wa kuwakopesha watanzania nyumba zenye ubora kwa gharama nafauu kwa mkopo wa muda wa miaka 25.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba, Bw. Ahmad Abdalla akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Benki ya PBZ, Dkt. Muhsin Masoud katika hafla ya kutiliana saini makubaliano kwa ajili ya kufanya uwezeshaji wa kuwakopesha watanzania nyumba zenye ubora kwa gharama nafauu kwa mkopo wa muda wa miaka 25.
……………………..
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeingia makubaliano na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa ajili ya kufanya uwezeshaji wa kuwakopesha watanzania nyumba zenye ubora kwa gharama nafauu kwa muda wa miaka 25.
Akizungumza leo February 7, 2024 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kutiliana saini makubaliano na Benki ya Watu wa Zanzinar iliyofanyika kwenye Jengo la Kambarage Upanga Makao Makuu ya NHC, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Bw. Ahmad Abdalla, amesema kuwa makubaliano hayo yanakwenda kuwasaidia watanzania kumiliki nyumba zenye ubora.
Bw. Abdalla amesema kuwa watanzania wengi wameshindwa kumiliki nyumba kutokana na kipato kidogo, hivyo Benki ya Watu wa Zanzinar imekuja kufanya uwezeshaji kwa kuweka utaratibu rafiki kwa watu wote ili waweze kupatiwa mkopo na kumiliki nyumba.
“Benki ya Watu wa Zanzibar itakupatia mkopo wa nyumba na baada ya kumaliza deni lako watakupatia hati ya Nyumba yako, haitaji uwe na dhamana ya kitu ili uweze kupata mkopo” amesema Bw. Abdalla.
Bw. Abdalla amesema kuwa utaratibu huu kila mtanzania ataweza kumiliki nyumba yake mapema, huku akiwapongeza Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kuungana na NHC katika kufanya uwezeshaji kwa watanzania.
Amesema NHC inatekeleza miradi mingi ikiwemo Samia Housing Scheme, huku akibainisha kuwa serikali baada kufanya maboresho ya sheria mbalimbali sasa imeleta ahueni kwa NHC kutekeleza kwa majukumu yake na kuleta tija kwa Taifa.
Bw. Abdalla amesema kuwa NHC imeendelea na utekelezaji wa kujenga Nyumba Bora kwa gharama nafuu katika maeneo mbalimbali lengo ni kuhakikisha watanzania wanamiliki nyumba zao kabla ya kustaafu.
Mkurugenzi Benki ya PBZ, Dkt. Muhsin Masoud, amesema kuwa benki ya PBZ ni Benki ya kizalengo ambayo imekusudia kuwasaidia watanzania.
Dkt. Masoud amesema kuwa benki ya PBZ ni miongoni mwa benki zenye riba nafuu kwani wanatoa riba ya asilimia 13 na kutoa fursa mtu kulipa ndani ya miaka 25 kulingana na uwezo wa mtu.
“Wakati huu sio wa kujenga kidogo kidogo tuchangamkie fursa ya kupata mkopo ili umiliki nyumba yako” amesema Dkt. Masoud.