Na: Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa-Dodoma.
“MSIDHANI katika awamu ya kwanza hapakuwa na rushwa. Rushwa ilikuwepo, lakini tulikuwa wakali! Tulitaka viongozi wetu watambue hilo, hatukufanya mchezo na rushwa hata kidogo! Na kiongozi akishathibitika amepokea rushwa, kazi hatukumuachia hakimu peke yake, Ehe viongozi wetu mnakula rushwa? (kicheko)!
Akishathibitika amekula rushwa, alihukumiwa kifungo kisichopungua miaka miwili jela, viboko ishirini na vinne; kumi na viwili siku anaingia gerezani na kumi na viwili siku anatoka, akamwoneshe mkewe (kicheko)!
“Wote wawili tuliwapa msukosuko, aliyetoa na aliyepokea, Wazanaki wanasema; ‘Bose manzi ga nyanja’ (wote wanasombwa na maji). Kwa hiyo hatukuwa na mzaha na rushwa hata kidogo.” Hayo ni maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati akimzungumzia tatizo la rushwa ambalo imenipendeza kulizingumzia leo katika safu hii.
Moja ya tafsiri ya neno ‘rushwa’ ni hali ya kutoa fedha au kitu ili kupata upendeleo. Kwa lugha nyingine ni hali ya kupata haki ambayo si yako na mara nyingi yule mwenye haki sawia anaikosa. Ndiyo maana Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipenda kusisitiza kwamba rushwa ni adui wa haki. Rushwa, kama kiini au sehemu ya ufisadi pia ina maana ya matumizi mabaya ya ofisi kwa maslahi binafsi. Yaani rushwa huwezi kuitenga na ‘umimi’ au ubinfasi. Hali ya kujali maslahi yako na tumbo lako lakini maslahi ya mwingine, wengine, jamii au hata nchi yako hayakuhusu!
Kwa tafsiri hizo, rushwa ni tatizo hatari la kijamii. Kuna watu wamepoteza haki, wamepoteza mali wamefungwa au kukosa maendeleo kwa ajili ya rushwa. Rushwa kubwakubwa zimesababisha kundi au kigenge cha watu wachache kuneemeka, wakasomesha watoto wao Ulaya huku jamii kubwa unayowazunguka ikitopea katika umaskini wa kutupwa.
Kutoka na athari hasi za rushwa, takribani kila nchi inafanya jitihada zake katika kupunguza au kukomesha rushwa kabisa. Kwa mfano, baada ya Marekani kuiondoa Uganda katika Mpango wa Ukuzaji wa Fursa za Biashara Afrika (AGOA) unaoiwezesha nchi hiyo kuingiza bidhaa bila vikwazo vya kiushuru Marekani, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema: “Kama Waganda tutashikamana na kudhibiti rushwa, hatua hii ya kunyimwa fursa za Agoa haitatukisa.”
Kwa hiyo Museveni analia rushwa kwamba unaweza kuyumbusha ustawi wa watu wake katika kipindi hiki cha kukosa fursa za Agoa huku akihimiza mshikamano. Tanzania si kisiwa, rushwa inaikabili pia nchi yetu na ndiyo maana juhudi mbalimbali zinafanyika kuhakikisha tunapunguza rushwa kwa kiwango kikubwa au kuimaliza kabisa.
Ipo methali isemayo “Usipoziba ufa utajenga ukuta.” Methali hii inatuhimiza kuwa tusiporekebisha jambo linapokuwa dogo, baadaye tatizo litakuwa kubwa sana na madhara yake yatakuwa makubwa zaidi. Pia methali hii inamaanisha ukidharau jambo dogo, linaweza kuongezeka na kuwa kubwa zaidi au usipozuia mambo madogo madogo yatakuwa mazito baadaye.
Ndio maana waswahili pia wanasema; mdharau mwiba, mguu huota tende.
Kutokana na uwepo wa rushwa katika maeneo mbalimbali kama vile mahakamani, hospitalini, ofisi za umma, shuleni/vyuoni na maeneo mengine, ni muhimu kuweka jitihada kubwa katika kuzuia (prevention) kuliko kupambana (combating) kwani gharama za mapambano ni kubwa sana kuliko za kuzuia. Vita ya rushwa ni jukumu la kila mwananchi na si serikali peke yake.
Ndiyo maana ni muhimu mno kuunganisha nguvu ya pamoja kupitia serikali na taasisi zake kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), asasi za kiraia na wananchi, ili kupiga hatua kubwa katika vita ya rushwa.
Desemba 4, mwaka 2023, akiwa kwenye kongamano la jukwaa la kitaifa la wadau dhidi ya rushwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maadili na Haki za Binadamu nchini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene alizitaka taasisi zinazohusika katika kusimamia utawala bora nchini, kujikita zaidi kuzuia rushwa badala ya kupambana nayo.
Simbachawene alikemea hali iliyopo sasa ya kupambana na rushwa kwenye miradi ya maendeleo badala ya kuzuia rushwa isitokee ili kupata thamani ya fedha (value for money) kwenye miradi hiyo ili kuleta tija kwenye maisha ya wananchi. “Wakati mwingine tunaweka nguvu kubwa na raslimali nyingi katika katika kupambana na rushwa wakati ambapo matokeo ya rushwa yanakuwa tayari yameshatokea na kuleta madhara kwa serikali badala yake tulipaswa kutumia nguvu hiyo hiyo katika kuzuia rushwa isiweze kutokea,” anasema Simbachawene.
Vilevile, Simbachawene alirejea kwenye tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini kuhusu hali ya utawala bora nchini ambapo tafiti zimebaini kuwa rushwa ni moja ya changamoto katika ufikiwaji wa lengo la serikali la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo katika sekta kama vile maji, afya, elimu na miundombinu. “
“Niwahakikishieni serikali yetu haitaacha kukabiliana na vitendo vya rushwa na kupambana inapobidi kwa kuwa zipo njia mbalimbali za kuzuia rushwa isiweze kutokea mojawapo ni hii ya kujadili pamoja mbinu za kuboresha zaidi usimamizi wa miradi ya maendeleo,” anasema Simbachawene.
Kutokana na tafiti kuonesha rushwa inaathiri ufikiwaji wa maendeleo ya wananchi, hivyo basi ni muhimu kuzuia rushwa ili kuepuka kadhia hii ambayo inaathiri maisha ya wananchi kutokana na miradi kutekelezwa chini ya kiwango au wananchi kukosa kabisa miradi ya maendeleo ambaye kama ingetekelezwa ipasavyo, ingeweza kuboresha hali za maisha za wananchi na kuchochea kasi kubwa ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi na nchi kwa ujumla.
Ni muda mwafaka sasa kuhakikisha kuwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kanuni na sheria zote zinazingatiwa ili kuondoa mianya ya rushwa. Mathalani, upatikanaji wa mzabuni wa kutekeleza miradi ya maendelo, apatikane kwa uwazi na akidhi vigezo vyote. Vilevile, hata baada ya kushinda zabuni hiyo, mzabuni afuate sheria za manunuzi kikamilifu katika utekelezaji wa mradi ili mradi uakisi thamani ya fedha na wananchi wafurahie mradi huo.
Kama hatutaziba nyufa za kutenda haki kwa wazabuni wanaotekeleza miradi ya maendeleo na kufuatilia ubora wa kazi, ni dhahiri watapatikana wazabuni wasiokidhi vigezo na hivyo kutekeleza miradi chini ya kiwango, ambapo itakuwa ni upotevu wa fedha za umma na kuwakosesha wananchi miradi yenye ubora. Ni lazima ieleweke kuwa gharama ya kuzuia rushwa ni ndogo kuliko ya kupambana nayo. Uchaguzi ni wetu, kutumia gharama ndogo kuzuia au kutumia gharama kubwa katika mapambano.
Nchi yetu bado ni maskini, bila kuzuia rushwa, wananchi wa chini ambao ni wengi watapata shida kupata haki zao. Kila mwananchi awe wa kipato cha juu, kati au chini anapaswa afurahie kuishi Tanzania kwa kupata haki bila rushwa. Usipoziba ufa utajenga ukuta. Tusifike huko kwenye mapambano ya rushwa, tunayo nafasi ya kuziba nyufa sasa na kujenga mwelekeo mzuri wa nchi yetu kwa maendeleo endelevu. Mtoa rushwa na mpokea ‘wote wasombwe na maji’ mara moja.
Dk. Reubeni Michael Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilayani Kongwa jijini Dodoma. Maoni: 0620 800 462.