Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejiment ya utumishi wa umma na utawala bora ,George Simbachawene akifungua kikao kazi hicho mkoani Arusha leo.
Mkurugenzi mkuu wa serikali Mtandao Benedict Ndomba akizungumza katika kikao kazi hicho mkoani Arusha leo.
Baadhi ya wadau wa serikali mtandao wakiwa katika kikao hicho mkoani Arusha.
…….
Happy Lazaro, Arusha
Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejiment ya utumishi wa umma na utawala bora ,George Simbachawene amezitaka taasisi zote za umma nchini kuhakikisha zinaingia kwenye mfumo wa serikali mtandao( e-GA) ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi unaoendana na sayansi na teknolojia na hatimaye wananchi kuweza kufikiwa na huduma kwa urahisi popote pale walipo.
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akifungua kikao kazi cha 4 cha wadau wa serikali mtandao kinachofanyika kwa muda wa siku tatu mkoani Arusha.
Simbachawene amesema kuwa,ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha inaingia kwenye mfumo huo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati kwani hilo ndo jukumu kubwa linalotakiwa.
Amesema kuwa ,kazi ya serikali mtandao ni sehemu ya kutoa huduma nzuri kwa wananchi huku akiwataka kufanya kazi kwa kusimamia mifumo hiyo na hatimaye wananchi kuweza kutatuliwa changamoto zao.
“Swala la Taasisi za umma kuingia katika mfumo huo ni lazima kwani mfumo huo unasaidia sana katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati sambamba na kupunguza foleni kwa wananchi katika kupata huduma hiyo,hivyo ni wajibu wetu kushikamana wakati wa utoaji wa huduma hizo .”amesema Simbachawene.
Aidha amezitaka taasisi hizo kuweka udhibiti wa kutosha katika upotevu wa fedha za umma ili kuokoa upotevu huo na hatimaye malengo yaliyowekwa yaweze kufikiwa kwa wakati .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa serikali mtandao Benedict Ndomba amesema kuwa, majukumu makuu ya taasisi za umma ni kuratibu na kukuza jitihada za serikali mtandao sambamba na kutoa ushauri.
Amesema kuwa, mamlaka imefanikiwa kujenga mfumo mzuri na taasisi za umma ambapo wamefanikiwa kuunganisha taasisi nyingi na mfumo huo na zinafanya kazi kwa weledi na mafanikio makubwa yameweza kuonekana.
Naye Makamu Mwenyekiti wa bodi ,Dkt .Jasmine Tiisekwa amesema kuwa ,kikao hicho kimeshirikisha zaidi ya wadau elfu moja wa serikali mtandao kutoka mikoa mbalimbali kwa lengo la kuweza kujadili mafanikio pamoja na changamoto mbalimbali na kuweza kuweka maboresho zaidi.
Tiisekwa amesema kuwa,kupitia kikao hicho wataweza kujadili namna bora ya kukuza serikali mtandao sambamba na kujadiliana kuhusu taarifa mbalimbali zinazohusu mamlaka hiyo .
“Nampongeza sana Rais Samia kwa namna ambavyo anaweka juhudi katika Tehama hususani katika utoaji wa huduma na kuweza kuwafikia wananchi kwa haraka sambamba na kutatua changamoto zao na hatuna budi na sisi kuhakikisha tunamuunga mkono Rais katika juhudi hizo “amesema