Na Sophia Kingimali
Serikali kupitia mradi wa ubia kati serikali na sekta binafsi(PPP) -TANROADS umepokea zabuni tatu kutoka sekta binafsi kwa lengo la kuzishindanisha na kupata mzabuni mmoja kwa ajili ya ujenzi wa barabara za haraka(Expressway) kutoka Kibaha,Mlandizi hadi Chalinze yenye urefu kilometa 78.9.
Akizungumza leo februari 6,2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua zabuni hizo mkurugenzi mtendaji wa kituo cha ubia (PPP)David Kafulila amesema ujenzi wa barabara hizo utasaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwani watu watatumia muda mfupi kufika kwenye maeneo yao ya uzalishaji.
“Kujengwa kwa barabara hizi hapa nchini zitachochea kasi kubwa ya maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla kwani utachukua muda mfupi njiani na muda mrefu utatumika katika kufanya kazi hii ni hatua kubwa sana kwa serikali katika kuendelea kuchochea maendeleo kwa nchi”amesema Kafulila.
Amesema ujenzi wa barabara hizo kwa mfumo wa ubia hauondoi mpango wa serikali kuendelea kuhudumia barabara zake lakini utasaidia fedha za serikali ambazo zingejenga barabara hizo zitatumika katika shughuli nyingine za kijamii.
Akizungumzia ujenzi wa barabara hizo kwa ubia amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanzia kibaha mpaka Dodoma ambapo awamu ya kwanza utaanzia Kibaha,Mlandizi Chalinze na Morogoro ambayo inaurefu wa kilomita 205.
“Mradi huu wa PPP utakuwa kwa awamu mbili ambapo sehemu ya kwanza itakua kibaha,Mlandizi na Chalinze kilomita 78.9 na sehemu ya pili itakua Chalinze mpaka Morogoro kwa urefu wa kilomita 126.1 na upembuzi yakinifu sehemu ya kwanza umefanywa na kukamilika Februari 2023 huku upenbuzi yakinifu kwa ajili ya kipande cha pili unaendelea”Amesema Kafulila.
Aidha Kafulila ameongeza kuwa barabara hizo zitasimamiwa na mbia na zitakuwa za kulipia na hailazimishwi kwa mtumiaji kutumia njia hizo kwani njia zote yaani barabara zinazohudumiwa na serikali na hizo za haraka zitakuwa zinafanyakazi hivyo ni hiyari ya mtu kutumia.
“Hizi barabara zinasimamiwa na mbia na hazitakuwa bure lakini zinarahisisha kwani ukinyoosha umenyoosha ni moja kwa moja mpaka unapoenda hapo hakuna hata kizuizi cha kukuzuia ili usimame hivyo mtu atachangua mwenyewe njia gani inamfaa kutumia maana zote zitakuwa zinafanyakazi kwa pamoja”Amesema.
Kwa upande wake meneja miradi ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi Mhandisi Kitainda Michael amesema wabia hao wamepatikana kwa mchakato wa wazi ambao serikali uliuweka ambapo kampuni tisa ziliomba tenda hiyo.
Amesema kamati ya kupitia nyaraka hizo(evaluation Committee)ilifanyakazi yake na kupitisha kampuni tano kati ya tisa waliowakilisha nyaraka za awali na kati ya kampuni hizo tano zilizorudisha nyaraka ni kampuni tatu ambazo ndizo zinashindanishwa ili kupatikana kampuni moja kwa ajili ya kukabidhiwa mradi huo.
“Leo tunafanya ufunguzi wa hizi zabuni baada ya ufunguzi tutaendelea na taratibu za uchambuzi na mwisho tunatarajia kumpata mwekezaji mzuri atakaepewa jukumu la kutekeleza mradi huu wa sehemu ya kwanza Kibaha hadi Chalinze(kilomita 78.9) Amesema Mhandisi Michael.
Muda wa ujenzi wa mradi huo unakadiliwa kuwa miaka mitatu huku muwekezaji ataendesha mradi huo kwa miaka 30 ambapo akikamilisha muda huo mradi utarudi kwa Serikali ya Tanzania na matarajio ni ujenzi wa njia za haraka kutoka kibaha hadi Dodoma ambapo mradi huo utatekelezwa kwa awamu.