Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bw. Ismail Seleman akizungumza na waandishi wa habari leo February 6, 2024 wakata akitoa taarifa ya utendaji kazi katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2023 hadi Desemba 2023.
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia miradi minne yenye thamani ya zaidi ya shillingi bilioni 7 ikiwemo mradi ujenzi wa kituo cha Afya cha Kinondoni ambapo umeshindwa kukamilika kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo February 6, 2024 wakata akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2023 hadi Desemba 2023, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bw. Ismail Seleman, amesema kuwa katika ujenzi wa kituo cha afya kinondoni wenye thamani ya sh. 1, 641, 561, 979.60 mkandarasi ameomba aongezewe muda ili aweze kukamilisha.
“Ufatiliaji wa karibu unaendelea kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha” amesema Bw. Seleman.
Bw. Seleman amesema kuwa pia wamepokea malalamiko 51 yaliyohusu rushwa ambapo yanaendelea kushughulikiwa katika hatua mbalimbali ili yapatiwe ufumbuzi.
Amesema kuwa malalamiko hayo alikuwa yanahusu tuhuma zilizopo katika sheria ya kuzuia n Kupambna na Rushwa (PCCA) pamoja na sheria nyengine (OL).
“Tuhuma zote zinafanyiwa uchunguzi wa awali kabla ya kutoa ushauri kwa walalamikaji, ni muhimu kufanya uchunguzi wa awali kabla ya kutoa ushauri kwa walalamikaji” amesema Bw. Seleman.
Ameeleza kuwa katika utekelezaji wa programu ya takukuru rafiki wamezifikia kata nne kupitia vikao na wadau na kufanikiwa kuzipatia ufumbuzi wa kero mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, kufanya semina 26, uimalishaji wa klabu za wapinga rushwa sita.
Bw. Seleman amesema kuwa katika kuhakikisha Takukuru Mkoa wa Kinondoni inatoa huduma na kuwafikia wananchi wote, wameendelea na utekelezaji wa programu ya TAKUKURU – Rafiki kwa kuendelea ushirikiano na jamii pamoja na wadau wanaohusika na kutoa au kupokea huduma, kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali.
“Tunatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Takukuru na kuwasihi wapatapo taarifa za rushwa kutoa taarifa kupitia mitandao yote ya simu kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba ya dharula 113, Kuzuia rushwa ni Jukumu lako na Langu; Tutimize wajibu Wetu” Bw. Seleman.