Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na kufikisha kwenye vituo teule vifaa vya TEHAMA vilivyogawiwa kwa vituo zaidi ya 800 kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).
Mchengerwa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa vituo vya walimu na Shule za awali na Msingi uliofanyika Jijini Dodoma.
“Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri imarisheni ulinzi na usalama katika shule zitakazopokea vifaa vya TEHAMA na ndani ya siku tatu vifaa hivi viwe vimekabidhiwa kwa mikoa husika.
Amewataka kuhakikisha shule zinazopelekewa vifaa zisibadilishwe labda kwa kibali maalumu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka watendaji hao kusimamia matumizi ya vifaa hivyo ili kuleta mapinduzi makubwa katika eneo la ujifunzaji na ufundishaji na kwamba yeye mwenyewe atapita kukagua utekelezaji wake lakini pia matarajio ya Serikali ni kuongeza vifaa zaidi ili shule zote ziweze kufikiwa.
Mchengerwa amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za dhati katika kuboresha sekta ya elimu nchini
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Franklin Rwezamula ameipongeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kununua vifaa vya TEHAMA kupitia Mradi wa Kukuza Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) kwa lengo la kuimarisha vituo vya walimu (TRC) na shule zilizoteuliwa kama sehemu muhimu ya kutolea Mafunzo endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) na kuwezesha zoezi la Ufundishaji na Ujifunzaji kwa wanafunzi ambao watatumia vituo hivyo zaidi ya 800
Aidha, amesema Wizara ya elimu itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 ambayo sasa ipo katika utekelezaji wake kwenye mitaala iliyoboreshwa hapa nchini.
Akitoa shukrani zake kwa Serikali mwanafunzi wa shule ya Msingi Mtemi Mazengo Valikaeli Mfinanga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kujifunzia masomo ya sayansi kwa vitendo kwa kuwa vitawasaidia kuwa na ukurasa mmoja na wanafunzi wengine ndani nje ya Tanzania na kupata ujuzi na maarifa mbalimbali.
Mradi wa uboreshaji wa elimu ya awali na msingi (BOOST) mpaka sasa umejenga shule mpya 302 za awali na msingi ofisi za walimu, mabweni na matundu ya vyoo.