Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Amani Kichama Fransisca Camilius Clement akikabidhi vitu mbalimbali kwa watoto wa kituo cha kulelea mayatima (Assalam Orphans Center ) Mpendae ikiwa ni shamrashamra kuelekea kutimiza miaka 47 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ifikapo fuabuari 05.
……………………..
Wilaya ya Mjini. 02/02/2024.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Amani Kichama Fransisca Camilius Clement ameitaka jamii kuwasaidia Watoto Mayatima kuwatatulia matatizo mbalimbali yanayowakabili ili wajihisi kuwa sawa kama Watu wengine.
Ameyaema hayo wakati wa kukabidhi msaada wa Mchele, Unga, Sukari, Mafuta ya kula na Taula za kike kwa Uongozi wa kituo cha kulelea Mayatima cha Assalam Orphans Center Mpendae ikiwa ni maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ameupongeza Uongozi wa kituo hicho kwa kujitolea kwa hali na mali kuwalea Watoto katika Maadili mema na kusema pengine bila ya kituo hicho wengelikuwa wakidhirura Mitaani.
Hivyo amewaomba Wafadhili na Watu wenye Uwezo kujitokeza kwa wingi kuwasaidia sambamba na kuahidi kuwa nao bega kwa bega katika kutafuta njia za kuwasaidia.
Kwa upande wake Katibu UWT Wilaya ya Amani Kichama Rabia Suleiman Kunambe amewataka Wananchi kuiga mfano wa kituo hicho kwani wamekuwa wakijitolea kuwalea Watoto hao kwa kuwapatia elimu ili waweze kuwa Viongozi wasuri hapo baadae.
Hata hivyo amesema wameamua kufika katika kituo hicho kwa kuwafariji na kuwapa moyo ili wasijihisi kuwa wametengwa na jamii baada ya Wazee wao kufariki.
Mapema akitoa maelezo Mkuu wa Kituo cha kulelea Mayatima Mpendae Khadija Khamis Hamdan amesema wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo Ukosefu wa Usafiri wa kupeleka Watoto Skuli na Ukosefu wa jengo.
Amesema kwa mpaka sasa wanatumia Jengo la kukodi ambalo linawasababishia gharama kubwa na kuwaomba UWT kuwatafutia ufadhili wa kujenga Jengo katika Kiwanja chao.