Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema tasnia ya Habari ni miongoni mwa tasnia zilizovamiwa na baadhi ya watu ambao hawana sifa hali inayosababisha kuididimiza tasnia hiyo yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Kanali Thomas ameyasema hayo mjini Songea, baada ya kusikiliza kero,maoni na mapendekezo ya wanahabari wa Mkoa wa Ruvuma ikiwa ni ratiba yake inayoendelea na kukutana na makundi mbalimbali kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
“Kuendelea kuwa na wanahabari wasiokuwa na sifa ni kuididimiza tasnia,leo hii serikali inatangaza ajira kwa wanahabari zikiwemo za maafisa Habari,kama una elimu ya cheti huwezi kuajiriwa,kama una cheti nenda kasome upate diploma na degree ,unaweza kujiunga na Chuo Kikuu Huria, unafanya kazi zako huku unaendelea na chuo’’,alisisitiza.
Amesisitiza kuwa taaluma ya Habari inabadilika kila siku hivyo ili kuendena na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni lazima wanahabari kujiendeleza kielimu.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewataka wanahabari wanapoandika Habari kuzingatia usalama wa Mkoa na Taifa ambapo amewakumbusha kuandika Habari kwa kuzingatia sheria na maadili ya uandishi wa habari.
Amekemea baadhi ya tabia ya wanahabari kutishia watendaji kuwaandika vibaya,pale wanaposhindwa kuwawezesha ambapo amesema kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya kazi.
Mkuu wa Mkoa amewataka wanahabari kujenga mahusiano na wakuu wa Taasisi za serikali na binafsi na kwamba wasitumike vibaya kwa maslahi binafsi badala yake kalamu zao zitumike kwa maslahi ya Taifa.
Hata hivyo amewataka wanahabari kupigania haki zao kama wanavyopigania haki za watu wengine na kwamba ameahidi changamoto na mapendekezo waliyoyatoa atayafanyia kazi ili waweze kufanya kazi kwa tija na ufanisi .
Awali wanahabari walizitaja changamoto mbalimbali zinazowakabili kuwa ni zaidi ya asilimia 95 ya wanahabari mkoani Ruvuma hawajaajiriwa badala yake wanafanya kazi kama vibarua hivyo kutekeleza majukumu yako kwenye mazingira magumu.
Wameomba kuwe na mzunguko wa wanahabari kwenye ziara za kimkoa na kitaifa badala ya kutumia waandishi wachache ili kila Mwandishi aweze kunufaika na ziara hizo.
Waandishi wameomba maafisa Habari kuwa kiungo kwa waandishi na watendaji wa serikali katika ngazi za Halmashauri na Taasisi za serikali ili viongozi hao waweze kufikika kwa urahisi.
Licha ya changamoto hizo waandishi wa Habari wameipongeza serikali mkoani Ruvuma kwa kusimamia vema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za kilimo, afya, elimu,maji,miundombinu na sekta nyingine ambayo inaendelea kuwanufaisha wananchi