Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma imeipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa dhamira yake ya kuondoa migogoro ya Ardhi na kuwaondolea kero wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa na kiongozi wa kamati hiyo Donald Mejiti alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mejiti alisema “tunatoa pongezi za dhati kwako Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mkurugenzi wa Jiji kwa kuonesha nia ya dhati kupunguza na kuondoa kero kwa wananchi inayotokana na migogoro ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Maoni yetu Chama Cha Mapinduzi ni kwamba mkishapima maeneo wekeni utaratibu mzuri wa kuyalinda ili yasivamiwe. Kuna tabia ya wananchi kuvamia maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa kialali kwa wananchi na kung’oa ‘beacon’. Mwananchi mwenye eneo anapokwenda kuangalia au kulinda eneo lake hufukuzwa kwa mapanga na kutishia amani. Utaratibu huu utawaondolea usumbufu wananchi halali wanaodhulumia haki zao”.
Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pilly Mbaga alitoa pongezi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kulipa fidia na kutatua migogoro ya Ardhi. Alisema kuwa awali wananchi walikuwa wakienda kwa wingi katika ofisi za CCM kulalamikia migogoro ya Ardhi na madai ya fidia, idadi hiyo imepungua sana siku hizi. Aidha, alishauri kuwa maeneo ambayo hayajapimwa na halmashauri yaweze kupimwa ili kuondoa uwezekano wa kuvamiwa.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema kuwa wananchi waliotakiwa kulipwa fidia walikuwa 385 ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kumaliza migogoro ya Ardhi. “Wananchi 127 ndio walijitokeza kulipwa fidia. Rai yangu hao wananchi waliobaki wajitokeze ili waweze kulipwa” alisema Kayombo.
Akiongelea viwanja mbadala, alisema kuwa halmashauri ilikuwa na deni la viwanja mbadala 3,992. Viwanja 1,102 vimetolewa kwa wananchi na viwanja 2,890 bado wananchi wanadai ambavyo watapatiwa kufikia mwisho wa mwezi Februari, 2024.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma imefanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM.