Na Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa-Dodoma.
Tarehe 1 hadi 7 mwezi Agosti kila mwaka ni “Juma la Unyonyeshaji Duniani”. Kutokana na unyeti na umuhimu wa suala la unyonyeshaji kwa watoto wachanga, Umoja wa Mataifa umeridhia nchi zote duniani katika Juma hilo kukaa pamoja, kutafakari na kuchukua hatua kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji kwani una faida kubwa katika afya ya mwili na akili kwa mtoto mchanga na mama pia.
Wataalam wa afya wanaelekeza mtoto anapozaliwa, anapaswa kuanza kunyonyeshwa baada ya saa moja tangu azaliwe. Maziwa ya mama yana kinga hasa yale maziwa ya mwanzo yenye rangi ya njano. Ni maziwa yanayoonekana kama ni uchafu kwa kuyaangalia lakini yana kinga kubwa dhidi ya magonjwa kwa watoto. Maziwa yanampa mtoto kinga ya asili ya kupambana na magongwa awapo mtoto hadi ukubwani.
Mtoto mchanga anapaswa kunyonyeshwa kwa miezi sita mfululizo bila kupewa chakula chochote. Ni muhimu hili likazingatiwa sana na wanafamilia wote waliopokea mtoto baada ya kuzaliwa kwani suala la kunyonyeshwa linapaswa kutiliwa mkazo na wanafamilia wote wala si kwa mama peke yake. Katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo, chakula cha mtoto kinapaswa kuwa maziwa ya mama peke yake bila kuchanganya chakula chochote.
Hata kama mama anatamani ampe mtoto wake kitu kingine kama uji, sharubati nk, hapaswi kufanya hivyo kwani kwa kufanya hivyo anaharibu msingi wa afya bora ya mtoto kwa kukiuka kanuni bora za unyonyeshaji na afya kwa ujumla.
Baada ya miezi sita kupita, mtoto anaweza kuanza kupewa vyakula vingine huku shughuli ya unyonyeshaji ikiendelea hadi kufikia umri wa miaka miwili au zaidi ndipo mama anaweza akaacha kumnyonyesha mtoto wake na kuanza kumpa vyakula vingine. Umuhimu wa unyonyeshaji unaenda sambamba na uzingatiaji wa vyakula bora kwa mama anayenyonyesha ili vimsaidie kutengeneza maziwa bora ya kumpa mwanae mchanga.
Mama anayenyonyesha akikosa vyakula bora, atashindwa kutengeneza maziwa bora ambayo ni muhimu kwa afya ya mtoto wake. Familia nyingi zinajitahidi kumpa chakula bora mama anayenyonyesha kwa siku chache tu baada ya kujifungua na baada ya hapo mama hupewa vykula ambavyo haviendani na hali aliyokuwa nayo. Ni muhimu baba wa familia katika kipindi ambacho mke wake yupo katika hali ya ujauzito, akawa anaweka fedha kidogo kidogo za akiba ili zije kutumika katika kumpa matunzo bora mke wake baada ya kujifungua kwani vyakula bora kwa mama anyonyeshae huchangia pia katika afya bora ya mtoto.
Msingi wa afya na lishe bora ya mtoto ni kupewa maziwa ya mama kikamilifu. Mtoto aliyenyonyeshwa kwa kufuata kanuni bora za afya, atakuwa na afya bora ambayo itamsaidia katika makuzi yake na hata akili yake itakuwa bora zaidi kwani afya ya ubongo wa mtoto inategemea sana ulaji wa vyakula bora alivyopata katika ukuaji wake ikiwemo maziwa ya mama. Wataalam wa afya wanasema unyonyeshaji unamsaidia mwanamke kuepukana na saratani ya matiti.
Kwa mantiki hii si tu kuwa unyonyeshaji unampa afya bora mtoto ila pia unamsaidia mama anayenyonyesha kuepukana na magonjwa kama saratani ya matiti. Hivyo mwanamke kukwepa kunyonyesha kama inavyoshauriwa ni kujiweka katika hatari ya kupata saratani ya matiti.
Wataalam wa afya pia wanasema unyonyeshaji unaboresha mahusiano ya mama na mtoto. Unyonyeshji ni jambo ambalo linafanyika kwa ukaribu sana kati ya mama na mtoto. Hivyo kwa kadri mama anavyonyonyesha mtoto wake kwa muda mrefu kama inavyoshauriwa kitaalam, ukaribu na mahusiano ya mama na mtoto yanaimarika zaidi. Mtoto anapokuwa yupo katika matiti ya mama yake mara kwa mara akinyonyeshwa, mahusiano na mama yake yanaimarika maradufu.
Ipo mitazamo potofu kwa baadhi ya wanawake kuhusu unyonyeshaji. Baadhi ya wanawake wanaamini unyonyeshaji unaharibu muonekano na maumbile yao. Baadhi ya wanawake hunyonyesha kwa muda mfupi tu ili kuepuka matiti yao kulala na kuharibu muonekano wao. Jambo hili si sahihi. Wanawake wanyonyeshe kwa muda mrefu kwa ustawi bora wa afya na kinga za miili ya watoto wao. Wanawake wajali afya za watoto wao kuliko kuangalia muonekano wao, kwani afya bora ndio kipaumbele cha kwanza katika maisha ya mwanadamu.
Waajiri wazingatie sheria za kazi na mahusano kazini kwa kuwapa masaa mawili kati ya masaa ya kazi wanawake wanaonyonyesha kupata muda wa kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo. Pia wanaume ambao wake zao wamejifungua, waajiri wawape likizo fupi ya siku tano katika juma la kwanza ambalo mke wake kajifungua ili washiriki kwa ukaribu katika kuwahudumia wake wao.
Wanawake na familia kwa ujumla ziache zisingizio vya aina yeyote katika kukwepa unyonyeshaji. Watoto wanyonyeshwe kikamilifu kwa afya ya mtoto na mama pia.
Dk. Reubeni Michael Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa-Dodoma. Maoni: 0620 800 462.