Ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 za maji ukiendelea katika kijiji cha Ndelenyuma Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mhandisi Triphon Mwanangwa akiwaonyesha baadhi ya viongozi wa kijiji cha Ndelenyuma hatua za ujenzi wa tenki la maji linalojengwa kupitia mradi wa maji ya Ndelenyuma -Lutukila.
……..
Na Mwandishi Maalum, Madaba
Wananchi wa kijiji cha Ndelenyuma katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea,wameiomba serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kukamilisha kwa wakati ujenzi wa mradi wa maji wa Lutukila-Ndelenyuma unaojengwa katika kijiji hicho ili waweze kuondokana na adha kubwa ya huduma ya maji safi na Salama.
Aidha,wamemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kampuni ya Demotoclasa Real Hope kufanya kazi usiku na mchana ili aweze kukamilisha kazi haraka kwa kuwa, wamechoka kuendelea na mateso ya kutembea mwenda mrefu kila siku kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.
Mkazi wa kijiji cha Ndelenyuma Hatuma Mgeni alisema,tegemeo kubwa katika kijiji hicho ni chemchem za asili na visima vifupi vilivyochimbwa kwa mikono na wananchi wenyewe ambavyo kiangazi vinakauka na maji yake siyo safi na salama hasa wakati huu wa masika.
Alisema,mradi huo utakapokamilika na kutoa huduma ya maji utasaidia sana kupunguza muda wa kwenda vijiji vya jirani kuchota maji,badala yake watatumia muda mwingi kufanya shughuli za kujiletea maendeleo.
Emanuel Mgaya alisema, katika kijiji chao kuna changamoto kubwa ya maji safi na salama na baadhi ya vijana wanatumia fursa hiyo kufanya biashara ya kuuza maji ndoo ya lita 20 kwa bei ya Sh.500 hadi 1,000,lakini wakati mwingine maji hayo siyo safi na salama.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Stanley Ngailo,ameipongeza serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizoanza kutekeleza mradi wa maji ya bomba.
“kijiji hiki kuna changamoto kubwa nay a muda mrefu ya maji safi na salama,hivyo wananchi wanalazimika kununua ndoo moja ya lita 20 kwa bei ya Sh.1,000 gharama ambayo ni kubwa mno,tunaiomba serikai yetu tukufu iharakishe ujenzi wa mradi huu”alisema Ngailo.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Demotoclasa Real Hope ya Dar es slaam Novatus Mwaipopo,amehaidi kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa kwa kuwa kazi kubwa kama ujenzi wa tenki,chanzo na kulaza bomba zimefanyika na ameishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi wakandarasi wazawa.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Songea Triphon Mwanangwa alisema,mradi huo utawanufaisha zaidi ya wakazi 4,331 wa vijiji vya Ndelenyuma na Lutukila kwa gharama ya Sh.bilioni 1.6.
Alisema,mpka sasa mradi umekamilika kwa asilimia 65 na kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa banio la maji,ujenzi wa matenki mawili moja la lita 50,000 na lingine lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 za maji.ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji na uchimbaji wa mitaro na kulaza mabomba ya kusamba maji umbali wa kilomita 23.7.
Aidha alisema,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 1,123,200 kwa siku na mahitaji ya maji kwa wananchi wa vijiji hivyo ni lita 258,000.
Ametaja faida za mradi pindi utakapokamilika kupunguza magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasio safi na salama kama kipindu pindu,kuhara na kuwapunguzia wananchi muda wa kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kawaida.