Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuimalisha ulinzi na usalama kwa kuishirikisha jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako na operesheni ambapo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 03 kwa tuhuma za kupatikana na nyara za Serikali Meno 09 ya Tembo yenye uzito wa Kilogramu 20 bila kuwa na kibali.
Akizungumza Januari 31, 2024 na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP Gallus Hyera ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia watuhumiwa 03 wakazi wa Msia kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali meno ya tembo.
Watuhumiwa hao walikamatwa Januari 30, 2024 katika msako uliofanywa katika Kijiji cha Ibembwa kilichopo Kata ya Igamba, Wilayani Mbozi wakiwa wameficha meno ya tembo kwenye Begi waliloliweka ndani ya mfuko wa Sandarusi wakiwa kwenye harakati za kutafuta wateja.
Aidha katika upelelezi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa ni wawindaji haramu,wasafirishaji na wauzaji wa nyara za serikali, watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao wanajihusisha na uhalifu wa nyara za serikali kuacha mara moja kwani awatoweza kukwepa mkono wa sheria.