Na Sophia Kingimali
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Ilala imetoa rai kwa wakandarasi kukamilisha miradi wanayopewa kwa wakati ukupunguza gharama na kuwezesha nia njema ya serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Wito huo umetolewa leo januari 31,2024 jijini Dar es salaam na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ilala Sosthenes Kibwengo wakati akitoa taarifa ya utendaji katika kipindi cha octoba hadi Disemba 2023.
Amesema kufuatia ukaguzi waliofanya wa mradi wa ujenzi wa vyoo vya umma wenye thamani ya bilioni3.27 unaosimamiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) wamebaini kasoro kadhaa ikiwemo na kucheleweshwa kukamilika mradi huo kinyume na mkataba.
“Baada ya kufanya kikao kazi na DAWASA na kukubaliana maazimio ya utekelezaji kasiro zilizothibitika zimeendelea kurekebishwa na mkandarasi amekatwa kiasi cha shilingi 326,476,502.60 kama faini ya kuchelewesha kazi”Amesema Kibwengo.
Amesema wameendelea kushirikiana na Halmashauri ya jiji la Dar es salaam na kuwezesha fedha ambazo zilikusanywa kwa mashine ya POS kuwekwa kwenye akaunt ya Halmashauri hiyo ambapo ni kiasi cha shilingi 1,830,546,332 ambazo hazikuwakilishwa kwa muda mrefu.
Sambamba na hayo Kibwengo amesema wamefanya chambuzi mbili za mifumo ya usimamizi wa ukusanyaji na matumizi ya ada za huduma za usafi na ulinzi karika soko la karume ambapo walibaini makusanyo pungufu kwa asilimia 47 ya makisio ambapo kiasi cha shilingi 245,138,000 yamepotea kwa kipindi cha januari hadi Septemba 2023.
Amesema upotevu huo umetokana na mengi ambapo kati yake ni kutokuwepo na taarifa za uhakika za idadi ya wafanyabiashara waliopo sokoni hapo.
Akizungumzia huduma ya TAKUKURU RAFIKI amesema walifanya vikao katika kata 9 na wananchi waliibua kero 50 na kushauri namna ya kuzitatua ili kukuza utawala ubora,kuboresha utoaji huduma na kuzuia rushwa.
Akizungumzia Uelimishaji umma amesema wameweka nguvu kubwa katika kufikia kundi la vijana kwani ni chachu ya mabadiliko katika jamii hivyo vijana watasaidia kubadili fikra na kushiriki katika kuzuia rushwa na kukuza utawala bora.
Aidha amesema wametoa mafunzo maalum kwa walimu walezi 239 wa klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi na sekondari lakini pia waliendesha shindano la ujumbe mfupi(video clip) kwa wanafunzi wa shule za sekondari ilala.
“Tumeendesha shindano hilo la ujumbe mfupi kuhusu nafasi ya vijana katika kuzuia rushwa tumepokea jumbe 96 hii kwetu ni mafanikio makubwa kwani ndio kwanza tumeanza hata hivyo kiwango cha kuelimisha kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 300 ukilinganisha na kile cha robo ya mwaka 2022″Amesema.
Akizungumzia mikakati ya Januari hadi March 2024 amesema wataendelea kushirikisha wadau kuzuia rushwa kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,kutekeleza programu ya TAKUKURU RAFIKI na kuelimisha jamii kwa kupitia mikusanyiko mbalimbali ya kijamii