Naibu waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Khafidh akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya maradhi yasiopewa kipaumbele ambayo hufanyika kila ifikapo Januari 30 duniani kote,hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Mratibu wa maradhi yasiopewa kipaumbele Zanzibar dkt. Shaali Ame akitoa ufafanuzi kuhusu maradhi hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya maradhi yasiopewa kipaumbele inayofanyika kila ifikapo Januari 30 duniani kote,hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Zanzibar. (PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR)
….……
Na Fauzia Mussa, Maelezo. 30/01/2024.
Wizara ya Afya ya Zanzibar imesema itaendelea kuchukuwa juhudi mbalimbali za kupambana na maradhi yasiopewa kipaombele ili kuyatokomeza Nchini.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Hassan Khamis Hafidhi ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya maradhi yasiopewa kipaombele Duniani huko Ukumbi wa Wizara ya afya Mnazimmoja Wilaya ya Mjini.
Amesema lengo la serikali katika kuchukuwa juhudi hizo ni pamoja na kuhakikisha kasi ya maambukizi ya maradhi hayo inafikia katika kiwango cha kuwa sio janga la jamii.
Amesema Wizara imeamua kuadhimisha siku hiyo kwa kuzungumza na waandishi wa habari ili kuweza kuifahamu siku hiyo na kupaza sauti kwa jamii iweze kuyafahamu maradhi hayo.
Alieleza kuwa katika kuongeza ufahamu dhidi ya maradhi hayo,Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) liliamua kuitambua siku ya tarehe 30 Januari ya kila mwaka kuwa ni siku ya maradhi yasiopewa kiapaombele (NTD) Duniani.
Aidha alifahamisha kuwa shirika hilo limedhamiria kutokomeza baadhi ya maradhi hayo ifikapo 2030, hivyo Zanzibar itaendelea kufuata miongozo na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na kuondoa maradhi hayo ili kuendana na azma na malengo yaliopangwa na Shirika hilo.
Mbali na hayo Mhe. Hassan ameitaka jamii na sekta nyengine ikiwemo sekta ya maji, kilimo, mifugo na mazingira kuunga mkono juhudi hizo ili maradhi hayo yaweze kuondoka katika jamii.
“Kusambaa kwa maradhi katika jamii yoyote inategemea sana na tabia za wanajamii husika,hivyo ni wajibu wetu kila mmoja kuhakikisha anaepukana na tabia hatarishi zinazopelekea kupata na kusambaza maradhi, bado baadhi ya wananchi wanatumia maji ya mito au mabwawa licha ya kuwepo kwa vyanzo vya maji safi na salama kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kufua, kukoga, kuosha vyombo jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya kichocho.”. alisema Naibu Waziri huyo.
Akizungumzia hali ya maradhi hayo Mratibu wa maradhi yasiopewa kipaombele Zanzibar Dkt. Shaali Ame amesema wizara ya Afya imeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya kichocho kutoka asimilia 8.1 (2012) hadi asilimia 1.7 (2019) pamoja na kupunguza maambukizi ya Ugonjwa wa Matende hadi kufikia chini ya asilimia 1:(<1%).
Alifahamisha kuwa kupitia wizara hiyo mikakati mbalimbali ya kupambana na maradhi hayo ikiwemo kutoa dawa kinga kwenye jamii na Maskulini, kupambana na konokono, kutoa elimu ya afya, kuhamasisha usafi wa mazingira , ujenzi na utumiaji wa vyoo pamoja na kufanyakazi na Sekta nyengine mbalimbali inatekelezwa ili kutokomeza magonjwa hayo.
Hivyo aliwataka wananchi kutumia dawa zinapotolewa kwenye jamii na kufuata njia nyengine za kujikinga na maradhi hayo ili kuyaondosha Zanzibar.
Alisema maradhi yasipewa kiapombele yanasababishwa na vimelea aina tofauti na kufahamisha kuwa miongoni mwa maradhi hayo ambayo yanaisumbuwa sana Zanzibar ni pamoja na kichocho, minyoo ya Tumbo na Matende.
“Katika visiwa vyetu vya Zanzibar, uwepo wa maradhi haya umetafautiana baina ya Kisiwa na Kisiwa (Unguja na Pemba) au Wilaya na Wialaya mfano hakuna maambukizi ya Kichocho kwa Wilaya ya Kusini Unguja lakini katika Wilaya hiyo kuna kiasi kikubwa cha maambukizi ya Matende ikilinganishwa na Wilaya yengine za Zanzibar,vilevile kuna kiasi kikubwa cha maambukizi ya Minyoo huko Kisiwani Pemba ukilinganisha na Unguja tafauti hii ya uwepo wa maradhi ndani ya Visiwa vyetu inatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kimaumbile” alifahamisha Mratibu huyo.
Siku ya Maradhi yasiopewa kipaumbele duniani ilitambuliwa rasmi kwenye mkutano wa 74 wa mwaka (World Health Assembly [WHA 74] (18)) uliofanyika Mei 31 ,2021, na kwa upande wa Zanzibar kwa mara ya kwanza inaadhimisha siku hiyo mwaka 2024 iliyoambatana na kauli mbiu “ungana,chukuwa hatua kutokomeza.”