Na Eleuteri Mangi, WANMM
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Lucy Kabyemera amekutana na wadau wa mipango miji ambapo wamejadili rasimu ya marekebisho ya Kanuni za Sheria za Mipango Miji nchini ili ziendane na hali ya sasa.
Akifungua kikao hicho Januari 30, 2024 jijini Dodoma, Naibu Katibu Bi Kabyemera amesema kuwa ardhi inahitaji kupangwa, kupimwa na kumilikishwa na kuendelezwa ikiwa katika hali nzuri kiuchumi, kijamii na kimazingira.
“Natambua ili kufanikisha azma hii, tunahitaji kuwa na kanuni sahihi za kuongoza upangaji wa miji yetu pamoja na matumizi mbalimbali ya ardhi hapa nchini” Naibu Katibu Bi Kabyemera.
Upangaji miji unaongozwa na Sheria ya Mipango Miji sura Na. 355 na Kanuni zake za mwaka 2018 ambazo zinahitaji kuboreshwa kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kimazingira, mitazamo ya kimaisha, kimaendeleo pamoja na mitazamo ya kimataifa vimekuwa msingi wa kupitia upya kanuni hizo ili ziendane na hali ya sasa.
Wadau hao ni pamoja na menenimenti ya wizara, Makamishna wa Ardhi Wasaidizi kutoka mikoa ya Tanzania Bara, wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali, taasisi za Serikali pamoja na zisizo za Serikali.