Mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 Timu ya Taifa ya Ivory Coast imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuwatoa Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo Senegal kwa Jumla ya Penati tano kwa nne katika mchezo wa hatua ya 16 bora.
Senegal walianza kupata goli mapema katika dakika ya nne kupitia kwa mchezaji wao Diallo.
Walifanikiwa kuendeleza faida hiyo kwa ulinzi mkali wa Simba wa Teranga hadi dakika ya 86 ambapo mchezaji wa Ivory Coast Kessie alifunga goli kwa mkwaju wa penalti na kusawazisha na kusababisha muda wa nyongeza kuongezwa.
Licha ya timu zote mbili kushindwa kufunga katika muda wa nyongeza, walielekea kwenye mikwaju ya penalti, ambapo wenyeji walipata faida.
Baada ya Niakhate kukosa penalti yake, Ivory Coast ilipata ushindi wa 5-4, na kutinga robo fainali na kuwaondoa bingwa wa sasa wa AFCON.
Katika mchezo mwengine timu ya Taifa ya Cape Verde nayo imefanikiwa kufuzu robo fainali baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Mauritania.