Mkurugenzi wa Huduma za Shirika,Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), CPA. Harold Basinda amewataka Maafisa Bajeti kutoka Idara na Vitengo na Vituo vya Utafiti vya Taasisi hiyo kuhakikisha uaandaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 unaendana na Mfumo wa kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS) na Mfumo maalum wa tathimini ya hali ya Rasilimali Watu Serikalini (HR Assessment).
Akizungumza wakati wa maandalizi ya mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025, mjini Babati, CPA Basinda amesema, mfumo wa PEPMIS ndio utatumika katika kupima utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja, kuzipima Idara na Vitengo, Kurugenzi, Vituo vya Utafiti pamoja na Taasisi kwa ujumla ambapo amesisitiza ni muhimu shughuli zitakazo bajetiwa kwa mwaka wa fedha ujao kuendana na mfumo huo .
Naye, Afisa Mipango wa TAWIRI, Bw. Joseph Anthony ameeleza maandalizi ya Mpango na Bajeti katika mwaka wa fedha 2024/2025 yanazingatia Mpango Mkakati wa Taasisi, vipaumbele vya kitaifa, mwongozo wa mpango na bajeti ya serikali, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2020-2025, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026.
Ikumbukwe, Vipaumbele vya TAWIRI ni kufanya tafiti za kimkakati na kusambaza matokeo ya tafiti kwa wadau, kutoa huduma za ushauri zinazohusu masuala ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori na afya ya mifumo ikolojia ya wanyamapori nchini , kuidadi wanyamapori katika maeneo yaliyohifadhiwa nchini, Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu na Ukarabati wa miundombinu chakavu ya Taasisi, Kujenga uwezo wa Taasisi kuendelea kutoa huduma na kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato, Kusimamia na kuimarisha miundombinu na mifumo ya TEHAMA / Teknolojia zinazohusu tafiti za wanyamapori.