Na Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa-Dodoma.
KWA mujibu wa mtandao wa Wikipedia; maadili ni mafundisho yanayotolewa katika nafasi mbalimbali, hasa katika malezi, ili kuelekeza binadamu atende namna ambayo inamjenga yeye na jamii nzima. Maadili yanajumuisha kanuni na imani zinazokubaliwa katika jamii.
Kwa lugha nyingine matendo yote yasiyokubalika katika jamii kama hii yetu ya Kitanzania yanapofanywa na mtu ni kwenda kinyume na maadili.
Matendo ya hovyo yako mengi, hii ni kuanzia mabaya zaidi na hatari (uhalifu) kama mauaji, ujambazi, ushoga na ubakaji hadi yanayoanza kuzoeleka katika jamii kama kula rushwa, wizi wa mali ya umma, ulevi wa kupindukia, kukosa heshima, kuvaa nusu uchi, kutukana, kubagua au kunyayasa wengine, kusengenya, kusema uongo na kadhalika.
Si jambo la kuficha kusema tunaishi katika jamii ambayo kwa kiasi kikubwa maadili yamemomonyoka sana na yanaendelea kumomonyoka. Kwa kuwa mimi ni mdau wa malezi na maadili kutokana na kuwa mwalimu kwa taaluma, nitaendelea kuzungumzia sana maadili na malezi. Hata hivyo, mmomonyoko huu wa maadili si tu upo kwa baadhi ya watoto na vijana, lakini pia hata baadhi ya wazazi na walezi, ambapo kimsingi wazazi na walezi ndiyo walipaswa kuwa kielelezo kizuri cha kuwalea watoto katika misingi ya maadili mazuri.
Kutokana na mmomomyoko wa maadili uliopo kwa sasa, jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kunusuru kikazi cha sasa na kijacho. Hofu ya Mungu, upendo na kudumisha undugu vimepungua sana badala yake ukatili, chuki, visasi vimechukua nafasi kubwa. Hapa kuna tatizo kubwa. Vyombo vya habari; runinga, magazeti na redio kila uchwapo vimekuwa vikitoa taarifa za uhalifu huu na ule katika maeneo mbalimbali ya nchini yetu.
Uhalifu huu umekuwa ukisababisha vifo vya watu, matatizo ya kisailojia ya kudumu, ulemavu au kukosa mali, hali inayorudisha nyuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Kujenga maadili mema ya mtu kunagusa wadau wengi, lakini msingi mkuu unaanzia katika familia.
Ninapenda kwa dhati kabisa kumpa kongole mwimbaji wa nyimbo za Injili, Daniel Thomas aliyetunga wimbo uitwao “Ibada Njema Huanzia Nyumbani” ambapo katika wimbo huo alisisitiza kuwa mambo mazuri kwa mtoto yanajengwa kuanzia nyumbani, yaani katika familia.
Mwimbaji Daniel katika wimbo huo alisisitiza kujenga kwanza mambo ya nyumbani kabla ya kujenga sehemu nyingine. Kwamba kushindwa kujenga maadili bora katika ngazi ya familia ndipo kunapoleta ugumu kwa walimu mashuleni, viongozi wa dini kwa waumini wao na viongozi wa serikali kwa watumishi na wananchi wanao waongoza.
Mtoto anapokosa msingi bora wa malezi yaliyojaa maadili mema katika ngazi ya familia, kumrekebisha kwingineko inawezekana lakini kunakuwa na ugumu kwelikweli. Ndio maana wahenga wakasema “samaki mkunje angalia mbichi”. Kwamba ukijaribu kumkunja wakati ameshakauka hakunjiki abadani, badala yake anakatika vipandevipande!
Hata maneno ya Mungu katika Mithali 22:6, Biblia inasema “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”. Mstari huu unaweka kielelezo cha kujenga tabia na maadili mazuri kwa watoto katika ngazi ya familia ambapo wazazi na walezi wanawajibika moja kwa moja kufanya jukumu hili.
Wanasaikolojia wanaamini kila mtu anazaliwa akiwa na tabia njema, hivyo anahitaji mwendelezo wa kulelewa katika malezi na maadili mazuri ili kuendelea kuwa na tabia na maadili mazuri. Waarabu wana msemo kwamba ‘Al-ummu madrasa’, wakimaanisha kuwa mama ni shule, ana wajibu mkubwa wa kumfanya mtu unayemwona mbele yako wakati unaposoma makala hii, awe kama alivyo; muungwana au mtu wa hovyo!
Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba ugumu uliopo wa kujenga tabia na maadili bora unaweza kupungua au kumalizika kabisa kama wazazi na walezi watatimiza kikamilifu jukumu la kulea watoto wao katika maadili yanayokubalika na jamii. Katika vitabu vyote vya dini, Mungu anawaagiza wazazi na walezi kuwafundisha watoto tabia na madili mazuri.
Katika Dini ya Kiislamu, kwa mfano, mafundisho yanaonesha wapo wazazi ambao siku ya Kiama watakuwa na thawabu za kuwawezesha kwenda peponi lakini watoto wao watapiga kelele mbele ya Mungu kwamba hawakuwakanya kuacha maovu na hivyo watashangaa kuona madhambi ya watoto wao yanakula thawabu zao na kujikuta wanaingia motoni.
Moja ya kozi niliyojifunza wakati nasoma Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Elimu ya Kikristo (Master of Arts in Christian Education) katika Chuo Kikuu cha Kikristo cha Elam (Elam Christian University) ni kozi ya “Utangulizi wa Elimu ya Kikristo – Introduction to Christian Education”. Katika kozi hiyo, nilijifunza historia ya maendeleo ya elimu ya dini wakati wa Agano la Kale, ambapo wazazi wa Kiyahudi walipewa jukumu la kuwafundisha watoto wao na watoto wa watoto wao (wajukuu) kuhusiana na elimu ya dini.
Pia, nyumbani kukawa sehemu muhimu ya mafunzo kwa watoto (The home became the most important place for instruction of children). Mstari wa kusimamia ulikuwa katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 6:6-9, Biblia inasema “Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako”.
Maagizo haya yalikuwa nyenzo muhimu ya kusaidia kujenga jamii yenye maadili mazuri ambayo ni jambo zuri hata mbele za Mwenyezi Mungu. Ukatili, ubakaji, mauaji ya kutisha, wizi na ujambazi ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili. Kama watoto watafundishwa maadili mema katika hatua za mwanzo kabisa za ukuaji wao, yaani kufundishwa nyumbani na wazazi au walezi wao kuna uwezekano mkubwa wa kujenga jamii yenye maadili mazuri.
Mtoto anayefundishwa huku akikemewa kujua kwamba kusema uongo ni kosa, kutoheshimu mwingine ni kosa, upendo kwa wengine ni lazima, ni muhimu kuheshimu mali ya mwingine, kusengenya ni kosa na mengine mfano wa hayo si rahisi kufanya matendo hatari kama ukatili, wizi na mauaji.
Vijana wanaojulikana kama ‘Panyarodi’ ambao wamekuwa wakifanya vitendo mbalimbali vya uhalifu yakiwemo mauaji ya watu wasio na hatia hawatakuwepo ikiwa watoto watalelewa katika maadili mazuri ya Kumcha Mungu huku juhudi hizo zikianzia katika ngazi ya familia. Ibada njema ya kuwafundisha watoto na vijana maadili na tabia njema ianzie nyumbani kwanza, ndipo baadaye iendelee katika nyumba za ibada, shuleni na sehemu nyingine.
Gharama za kujenga maadili mazuri kabla mambo hayajaharibika ni ndogo kuliko gharama za kujenga maadili baada ya mmomonyoko wa maadili kutokea. Ukiona inafikia mahala mtoto hamsikilizi mzazi wake, mtoto hamjali mzazi wake huku wengine wakifikia kuwatukana au kuwapiga kabisa wazazi wao, basi ujue wazazi haohao wanavuna walichopanda. Huo ndio ukweli mchungu!
Jamii tubadilike ili kujenga jamii yenye upendo, amani, utulivu na maendeleo kwa sababu tukifeli kujenga maadili na malezi mema nyumbani, tumefeli pakubwa mno. Tusifikie kwenye msemo wa Kiswahili wa ‘asiyefunzwa na mama, hufunzwa na ulimwengu’. Kwa nini mtoto afunzwe na ulimwengu? Ndiyo maana nasema, ibada njema ya kujenga maadili mena kwa mtoto, kama alivyoimba Daniel, inaanzia nyumbani na sio shuleni, ofisini, kanisani wala msikitini.
Dk. Reubeni Michael Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa-Dodoma. Maoni: 0620 – 800 462