*Ni la Mafuta Safi kutoka Dar es Salaam hadi Ndola Zambia
*Dkt. Biteko asema pia litanufaisha mikoa ya kusini
*Zambia yasema ipo tayari kutekeleza mradi huo
*Timu ya Wataalam yaanza majadiliano
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na Waziri wa Masuala ya Nishati wa Zambia, Mhe. Peter Kapala leo wamefanya kikao kilicholenga kujadili nia ya Serikali ya Tanzania na Zambia kuanza ujenzi wa bomba la inchi 24 la kusafirisha mafuta safi kutoka Tanzania kwenda Zambia.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 29 Januari, 2024 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Makatibu Wakuu wa Wizara za Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (Tanzania) na Dkt. Chisangano Zyambo (Zambia) pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Wizara hizo na Mashirika yanayosimamia Mafuta.
Dkt. Biteko amesema, majadiliano hayo ya Mawaziri yanatokana na ziara ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Zambia mwezi Oktoba mwaka 2023 ambapo katika mazungumzo yake na Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema walijadiliana kuhusu kuongeza uwekezaji kwenye Bomba la Mafuta la TAZAMA kwani bomba hilo kwa sasa halikidhi mahitaji kutokana na kuwa na ukubwa wa inchi 12.
“Kulingana na maendeleo makubwa katika nchi zetu mbili, mahitaji ya mafuta yamekuwa makubwa ndio maana inabidi kujenga bomba jingine jipya kubwa ambalo litasafirisha mafuta kutoka Tanzania kwani kuna Bandari, bomba hili litakalojengwa pembeni ya Bomba la Mafuta la TAZAMA litasafirisha mafuta pia kwenda mikoa ya kusini mwa Tanzania na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na kuwapatia wananchi mafuta ya gharama nafuu.” Amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa, bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,710 na uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 2.5 na kusisitiza kuwa, kwa uwekezaji huo kunahitajika umakini kwenye utekelezaji wake na bila kuuchelewesha.
Ameongeza kuwa, bomba litakuwa na matoleo ya Mafuta katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Morogoro, Makambako, Mbeya na Songwe na kupunguza suala la mikoa hiyo kutegemea kupakua mafuta jijini Dar es salaam pekee.
Dkt, Biteko amesema kuwa, Timu ya Wataalam wa majadiliano inaanza kazi leo na hii ikiwa ni msukumo ambao Marais wa nchi zote mbili wamekuwa wakiutoa ili kutekeleza mradi huo.
Ameeleza kuwa, Serikali ya Tanzania, ipo tayari kutekeleza mradi huo wa kimkakati na hii ikizidi kuonesha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili ambao umepelekea utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo wa bomba la TAZAMA na mradi wa usafirishaji umeme kutoka Tanzania kwenda Zambia wa kV 400.
Kwa upande wake, Waziri wa Masuala ya Nishati wa Zambia, Mhe. Peter Kapala amesema kuwa, nchi hiyo inauhitaji sana mradi huo na Rais wa nchi hiyo anaupa msukumo na anatarajia kwamba kazi ya utekelezaji itafanyika kwa kasi na umakini ikitarajiwa kuwa mradi ukamilike kwa muda wa miaka miwili.
Ameeleza kuwa, kampuni nyingi zimeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo ametanabaisha kuwa nia za makampuni hayo zitafanyiwa tathmini na wataalam ili kupata kampuni bora.
Ameongeza kuwa, mahitaji ya mafuta nchini Zambia yanazidi kuongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za maendeleo nchini humo ikiwemo uanzishwaji wa migodi ya madini ya shaba hivyo Serikali ya Zambia ipo tayari kutekeleza mradi huo.