NIRC Manyara.
Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji inayoendelea kutekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji nchini ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Umwagiliaji la Tlawi lililopo katika kijiji cha Tlawi halmashauri Mbulu mji mkoani Manyara.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mradi wa Umwagiliaji Tlawi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Henry Mahoo ambapo amekiri kuridhishwa na utekelezwaji wa mradi huo huku akito ushauri kwa wataalamu kuzingatia eneo la mradi huo linabaki na miti ili kudhibiti uharibiu unaoweza kutokea kutokana maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amesema mradi wa ujenzi bwawa la Tlawi una thamani ya jumla ya shilingi bilioni 6.4 ambao unahusisha ujenzi wa bwawa pamoja na miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya wakulima yenye takribani hekta 90, ambapo utekelezaji wake hivi sasa umefikia asilimia 95.
Aidha Mndolwa amewaahidi wakulima wa skimu hiyo kutekeleza ombi lao la ongezeko la hekta 110 na kusisitiza wakulima hao kuendelea kuilinda miundombinu hiyo kwani miundombinu hiyo imejengwa kuwanufaisha wakulima hao.
Bodi hiyo pia imetembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya umwagiliaji ya Endagaw iliyopo halmashauri ya Hanang na kushauri wananchi kulinda vyanzo vya maji katika eneo la bwawa ili kuepusha kujaa kwa mchanga katika bwawa wakati Tume ikiendelea kutafuta mkandarasi mwingine kwa aajili ya kutekeleza mradi huo kutokana na mkandarasi wa awali kushindwa kukamilisha mradi huo.