Wastaafu nchini wameombwa kutumia mfuko wa hati fungani na Mfuko wa kujikimu iliyomo kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja Inayoendeshwa na UTT AMIS ili waweze kunufaika kwa kupata gawio la kila mwezi au miezi sita.
Ombi hilo limetolewa leo Jumamosi Januari 27, 2024 na Afisa mwandamizi kutoka UTT AMIS Bw. Rahim Mwanga wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na wahariri juu ya namna Mifuko hiyo inavyofanya kazi.
Mwanga amesema moja ya changamoto kubwa ya wastaafu ni namna Bora ya kutumia mafao yao lakini kupitia mifuko hiyo wanaweza kuwekeza na wakapata gawio la kila mwezi,miezi sita huku kupitia mfuko wa kujikimu wanaweza kupata gawio kila miezi mitatu au mwaka mmoja kulingana na uwezo wa mtu.
“Mifuko hii inamanufaa makubwa sana kwa wastaafu na inatoa magawiwo ya mara kwa mara kwa maana hapa tunalenga wawekezaji waliopata fedha za mkupuo na wanataka kupata uhakika wa kipato cha mara kwa mara maana mtu anapopata mafao yake anashindwa ayatumieje na wengine wanajikuta fedha zinaisha kabla ya kufanya jambo lolote hivyo niwaombe mjiunge na mifuko hii ili muweze kufaidi mafao yenu kupitia gawio” Amesema Mwanga
Ameeleza kuwa UTT AMIS wamekuwepo kwenye soko takribani miaka 20 na wanamifuko sita ya uwekezaji wa pamoja ikiwemo mfuko wa umoja,mfuko wa watoto,mfuko wa wekeza maisha,mfuko wa kujikimu na mfuko wa ukwasi ambapo kwa kipindi chote hicho wameweza kufanya vizuri kwenye soko na kutengeneza imani kwa wawekezaji wao.
“Kwa sasa tunawawekezaji laki tatu lakini tunarasilimali za mfuko zaidi ya tilioni 1.9 na faida kwa wawekezaji zimekuwa bora na kuongezeka siku hadi siku mfano juni 23 mifuko ilitoa faida ya wastani kuanzia asilimia 12-14 hii ni faida shindani na nzuri sana kwenye soko,hivyo wananchi wanaweza wakatumia mifuko kuwekeza akiba zao kukuza mitaji na hatimae wakaweza kushiriki kwa mapana kwenye shughuli mbalimbali za uchumi”, amesema
Aidha, amesema kunawatu wanamahitaji ya kukuza mitaji na biashara,kusomesha watoto, kununua viwanja vyote hivyo vinahitaji pesa na pesa ya mkupuo inakuwa ni changamoto kuipata lakini wanaweza kuanza kuwekeza kidogokidogo na wakakuza mitaji yao.