Na: Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kusema kuwa ili nchi iweze kuendelea na ipate maendeleo, inahitaji vitu vinne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Uwepo wa vitu hivi vyote vinne na mfumo madhubuti wa kuratibu, ni dhahiri maendeleo ya kweli yanayogusa maisha ya watu yataweza kufikiwa kwa mafanikio makubwa. Lengo la makala hii ni kuangazia jambo moja kati ya manne yaliyoainishwa na Hayati Baba wa Taifa – Siasa safi. Siasa ni maisha. Siasa inagusa kila eneo la maisha ya kawaida ya kila siku ya mwanadamu. Hakuna namna ambayo ustawi na maendeleo ya watu yanaweza kujadiliwa na kufikiwa bila uwepo wa siasa tena siasa safi yenye tija kwa wananchi.
Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wanasiasa nchini kushindwa kufanya siasa safi zenye kugusa maisha ya wananchi, badala yake kujikita kutoa lugha za kebehi, dharau na zisizo na staha. Siasa safi ni siasa zenye kujenga hoja, zenye kujikita kujibu mahitaji ya wananchi.
Oktoba 11, 2023 akiwa mgeni rasmi wa mkutano wa wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopokea taarifa ua utekelezaji wa Ilani ya CCM jimboni Chalinze ulioandaliwa na Mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alitoa darasa zuri la siasa safi kwa wanasiasa hasa wanaccm.
Dk. Biteko alisisitiza kwamba ili kuwa na maendeleo ni vema kufanya siasa za kubadili maisha ya watu badala ya siasa za maneno. “Shikamaneni, thaminianeni na kuvumiliana angalieni yanayowakeka pamoja badala ya yale yanayowatenganisha tusiingie kwenye matusi na kejeli kazi yetu iwe ya kuyasemea yale yaliyofanywa na serikali. Wananchi wanachohitaji ni huduma tuwapelekee maendeleo huko waliko raslimali fedha zilizopo zitumike kwa kiwango kinachotakiwa” alisisitiza Dk. Biteko. Hili ni darasa, hii ni shule kamili kutoka kwa Dk. Doto Biteko.
Dk. Biteko anafahamu kiu kubwa waliyonayo wananchi ni utatuzi kero zao na kugusa maisha yao kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo. Utatuzi wa kero za wananchi, unategemea utendajikazi madhubuti wa viongozi waliopewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi (viongozi wa kuchaguliwa), viongozi wa kuteuliwa na watumishi wa umma wanaowajibika moja kwa moja kuwatumikia wananchi katika maeneo yao ya kazi. Kwahiyo, viongozi wanawajibika moja kwa moja kufanya siasa za kubadili maisha ya watu ili kuchochea maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla.
Dk, Biteko anataka kasi ya uboreshaji wa huduma za kijamii kwa wananchi kwani hiyo ndiyo siasa safi yenye kubadili maisha ya watu. Wananchi wanataka huduma bora za kijamii kama vile elimu, afya, maji, umeme na nyinginezo. Pia wanahitaji kuboreshewa shughuli zao, mathalani, kupata pembejeo kwa ajili ya kilimo, mifugo an uvuvi. Vilevile, wananchi wanayo kiu ya kuboreshewa miundombinu ya barabara na ujenzi wa masoko ili waweze kufanya biashara zao katika mazingira mazuri ili hatimaye waweze kupata kipato kwa ajili ya familia zao na kuchangia maendeleo ya nchi yao. Kufanikiwa kwa haya yote yanategemea utendajikazi wa viongozi wenye dhamira ya dhati ya kubadili maisha ya watu wanaowaongoza na kuwatumikia.
Aidha, Dk. Biteko anatoa rai juu ya matumizi mazuri ya fedha za umma zinazotengwa na serikali katika kughramia miradi mbalimbali ya maendeleo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kubadili maisha ya watu yanakwenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi ambapo bila matumizi mazuri ya fedha hizo, miradi hiyo itakwama na hivyo maisha ya wananchi yataendelea kuwa duni. Hivyobasi, mkazo wa Dk. Biteko wa kutaka fedha za miradi itumike kwa kiwango kinachotakiwa ni namna bora ya kufanikisha mkakati wa serikali wa kubadili maisha ya wananchi wake kutoka maisha ya chini hadi maisha bora.
Kimsingi, kwa wanasiasa kutaka kuungwa mkono na wananchi bila kuwa na mikakati thabiti inayopimika ya kubadili maisha ya wananchi ni kupoteza muda tu. Wananchi wa sasa wanajua aina ya kiongozi wanayemtaka ili washirikiane nae katika juhudi za kujiletea maendeleo, kiongozi huyo ni yule anayefanya siasa zenye mrengo wa kuboresha maisha ya wananchi wake. Ushirikiano na mshikamano vilevile ni moja ya msingi muhimu wa kufanya siasa safi.
Viongozi ni lazima washirikiane kikamilifu na wananchi wao ili kuunganisha nguvu ya pamoja na hatimaye kufikia maendeleo ya kweli. Pengine, ni muda muafaka sasa kwa wanasiasa kubadili aina ya siasa. Wakati na mazingira ya siasa nchini yamebadilika. Ni lazima kujikita katika siasa safi, bila kufanya hivyo, wanasiasa wataangukia pua, kama hawaamini wajaribu waone.
Dk. Reubeni Michael Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.