Na Sophia Kingimali.
Naibu Spika na mbunge wa iIala Musa Zungu amezitaka Halmashauri na askari wa akina mgambo wa jiji kutowachukulia bidhaa wamachinga waliopanga kwenye maeneo yasiyo rasmi badala yake wawakabidhi bidhaa zao na kuwapa maelekezo sehemu sahihi ya kufanyia biashara zao.
Maagizo hayo ameyatoa leo jijini Dar es salaam wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zilizoandaliwa na wamachinga wa na taasisi ya Hatua kwa Hatua na Mama.
Amesema Rais ameweka mazingira mazuri kwa wamachinga hivyo hawatawavumili wanaoharibu taswira ya Rais kwa wananchi wake.
“Rais wetu ameboresha mazingira mazuri ya masoko yetu ili kusaidia wamachinga kufanya biashara zao kwa uhuru na usalama sasa mnapowanyang’anya hawa wamachinga mali zao ambapo mitaji yao yenyew ni midogo mnataka walipe faini wakapate wapi swala hilo kwa sasa hatulitaki ukimkuta kwenye mazingira ambayo sio rasmi muelekeze pa kwenda na si kuchukua biashara yake”amesema Zungu.
Aidha Zungu ameongeza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono wajasiriamali kwa kuendelea kuwapa mikopo ili waendelee kukuza biashara zao.
Nae mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema maisha ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan yamekuwa baraka kwa nchi na wananchi wake kwani ameweza kuwatumikia wananchi katika nyanja zote.
Amesema Rais amefanya mambo makubwa ambayo yamekuwa alama kwa wananchi kwani ameboresha Afya lakini pia ubora wa elimu na elimu bure kuanzia shule ya awali mpaka sekondari.
“Mama amefanya mambo makubwa sana kwa wananchi katoa huduma za afya nzuri zilizoboreshwa mama mjamzito anahudumiwa mpaka anajifungua na mtoto huyo anapofikisha miaka mitano anaingia shule bure anamaliza elimu yake ya sekondari”Amesema.
Sambamba na hayo amesema Rais ameboresha miundombinu ya barabara lakini pia ameendelea kudumumisha Amani na mshikamano na pia kuwezesha maridhiano na kukuza demokrasia.
Nae Mkurugenzi wa soko Machinga Complex Stella Mgumia amewataka wafanyabiashara wanaopanga barabarani warudi kwenye masoko ambapo ndio sehemu rasmi kwani Rais ameweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wote.
Aidha Mgumia amesema kuwa pamoja na mazingira yaliyowekwa wafanyabiashara wanapaswa kufuata sheria lakini pia kuweka mazingira safi na salama kwenye maeneo yao ya biashara ili kutunza miundombinu iliyopo lakin pia kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.
Nae mwenyekiti wa Machinga Namoto Namoto amesema Rais amejali sana wajasiliamali wadogo kwa kuwajengea masoko mengi na bora lakini kuwafanya waweze kukopesheka kwenye mabenki na kupelekea kukuza mitaji ya wamachinga hao.