Na Sophia Kingimali.
Naibu waziri wa Nishati Judith Kapinga amelitaka shirika la umeme TANESCO kuhakikisha wanarekebisha miundombinu yake nchi nzima ikiwemo transfoma ili kuepuka kuwasababishia usumbufu wananchi wa kukatika kwa umeme kunaposababishwa na ubovu wa miundombinu na si uhaba wa umeme uliopo.
Maelekezo hayo ameyatoa leo Januari 26,2024 jijini Dar es salaam wakati alipotembelea Transfoma mbalimbali zenye changamoto katika wilaya ya Temeke.
Amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme hivyo hawatavumilia yeyote atakaesabaisha uharibufu kwenye miundombinu hiyo.
“Nawaelekeza TANESCO hakikisheni mnafanya marekebisho kwenye transfoma zote nchini hatuwezi kuona transfoma la milioni 20 linaharibika kwa ajili ya kifaa cha shilingi laki 5″Amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa kitendo cha kukosekana vifaa vya ulinzi kwenye mifumo ya transfoma kutapelekea uharibufu mkubwa wa transfoma hizo lakini pia kunasababisha usumbufu kwa wananchi.
“Kwa sababu tunapitia changamoto ya upungufu wa umeme basi mnataka kunapitia humo kuleta sababu kumbe changamoto nyingine mnazijua ni kitendo cha kuwajibika kwa hili hatutalifumbia macho tunataka kazi na si sababu”amesema.
Ameongeza kuwa dhama zimebadilika hivyo wanapaswa kujitathimini na kufanyakazi kwa weredi ili kuwapunguzia lawama mafundi na mameneja wa wilaya na mikoa.
Sambamba na hayo amekitaka kitengo cha manunuzi TANESCO kupitia upya sheria na mikataba kwa Makandarasi wanaowapa tenda ya vifaa ikiwezekana kuwapa miezi sita baada ya miaka miwili ili wakionyesha ucheleweshaji wa kuleta vifaa kuachana nao na kutafuta wengine.
Kwa upande wake mkurugenzi wa TANESCO kanda ya Mashariki Mhandisi Keneth Boimanda amesema maelekezo yaliyotolewa watayafanyia kazi ipasavyo na kwa haraka.
“Maelekezo tumeyapokea tutakaa wote maenjinia na mafundi kuhakikisha tunatekeleza maagizo haya ya kuzifanyia marekebisho transfoma zote zenye hatari ya kuharibika”amesema Mhandisi Boimanda.
Nae,Mkuu wa wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda amesema TANESCO wanapaswa kuwajibika na si kutupiana mpira hivyo kama wilaya watasimamia ili kuona utekelezaji wa maboresho kwenye transfoma hizo.
“Kuna mahali tumefika lazima TANESCO wawajibike fyuse ndogo wanashindwa kununua kwa ngazi ya wilaya wanatupia mpira kwa makao makuu kwamba kitengo cha manunuzi ndio kifuatilie hii si sawa lazima wajitathimni sisi tutasimamia ili tuone maboresho maana serikali inajitahidi kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika hivyo miundombinu isiwe kikwazo inabidi TANESCO wafanyekazi wasimuangushe Rais wetu”amesema Mapunda.