Wakazi waishio pambazoni mwa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Mkoani Morogoro wamekiri kuwa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) umekuwa msaada mkubwa katika kukomesha ujangili wa Wanyamapori na ukataji miti ovyo katika Hifadhi ya Taifa Mikumi.
Akielezea Mafanikio yake baada ya kujiunga kwenye kikundi cha Benki ya Hifadhi za Jamii (COCOBA) Bw.Fadhili Issa amebainisha kuwa, huko nyuma alikuwa akijishughulisha na biashara ya ujangili ya Wanyamapori huku maisha yake yakiendelea kuwa yatabu lakini Sasa anamiliki Biashara yake ya kazi za Sanaa inayompatia fedha za uhakika za kuendeshea maisha ya familia yake.
Bw. Issa ametoa wito kwa baadhi ya watu wenye tabia za kufanya uwaribifu kwenye Hifadhi za Taifa ili kujipatia kipato kuachana na tabia hiyo kwa kuwa ni yakibinafsi maana Hifadhi za Taifa ni kwa manufaa ya watanzania wote na ni urithi kwa kizazi kijacho.
Akielezea Mafanikio ya yaliotokana na Mradi wa REGROW kwa jamii, Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS) Kijiji cha Mang’ula B Neema Mabiki, amesema, kupitia elimu aliyoipata, ameweza kuwaelimisha wanavijiji wenzake mbinu mbalimbali za kujilinda na wanyamapori wakali na waharibifu na namna umuhimu wa Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa kwao, hali iliyopelekea wananchi kudhamini uwepo wa Hifadhi hiyo yenye vivutia vya kipekee Duniani.
Serikali kupitia mradi wa REGROW unaotekelezwa kwa fedha za Mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, imeendelea kuwanufaisha wananchi hususani waishio pembezoni mwa Hifadhi za Taifa zilizopo Kusini mwa Tanzania kwa lengo la kuimarisha uhifadhi na utalii nchini.