Na Hellen Mtereko, Mwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan atakabidhi zana za uvuvi kwa wavuvi na vikundi mbalimbali katika Mikoa ya Kanda ya ziwa inayojihusisha na masuala ya uvuvi.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Januari 26, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ujio wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu anaetarajia kuwasili Mkoani hapa Januari 29 kwaajili ya shughuli ya kukabidhi zana hizo Januari 30 mwaka huu katika uwanja wa michezo Nyamagana.
Makalla amesema shughuli hiyo ya kukabidhi zana za uvuvi imeratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100.
“Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Mikoa jirani mjitokeze kwa wingi kuanzia kwenye mapokezi Januari 29 katika viwanja vya ndege na tarehe 30 kwenye uwanja wa michezo Nyamagana kwenye shughuli hiyo muhimu ya kukabidhi zana za uvuvi”, amesema Makalla