Na. Damian Kunambi, Njombe.
Ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya kuhamasisha mpango wa kuongeza kasi ya kupunguza udumavu kwa watoto mkoani Njombe Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kupitia mapato yake ya ndani imetenga fedha kiasi cha sh. Mil 33 zilizolenga kuchangia uboreshaji wa huduma ya lishe kwa watoto wilayani humo sambamba na kuweka mkakati wa kupita kijiji kwa kijiji ili kutoa elimu ya lishe.
Akizungumzia kutengwa kwa fedha hizo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius katika mkutano wa hadhara uliolenga kutoa elimu ya lishe bora kwa mtoto uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji wakiwemo viongozi wa dini na wananchi huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa zimeonyesha kuwa katika wilaya hiyo 47% ya watoto walio chini ya miaka mitano wilayani Ludewa wanakabiliwa na tatizo hilo la udumavu hivyo mkuu wa wilaya hiyo Bi. Victoria Mwanziva ameweka mkakati wa kupita kijijikwa kijiji na hasa katika maeneo ambayo yameonekana kuathirika kwa kiwango kikubwa na kutoa elimu.
“Ludewa tunazalisha vyakula vya kila aina ambavyo ni mtaji tosha katika kuhakikisha watoto wetu wanapata afya bora na kuondokana na udumavu, mimi na timu yangu tutapitakitoa elimu kila kona ya wilaya hii na kuhakikisha tatizo hili linakwisha”. Amesema Mwanziva.
Awali afisa lishe wa Ludewa akitoa takwimu za udumavu huo ameeleza miongoni mwa sababu zinazopelekea kuwepo kwa udumavu kwa watoto hao kuwa ni ulevi uliokithiri pamoja na mama kuanza kufanya shughuli za kilimo mapema na kupelekea kukosa muda wa kumpa mtoto huduma stahiki.
Hali hiyo imepelekea mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka kutoa rai kwa wananchi wote wa mkoa huo kuacha unywaji pombe uliokithiri lakini pia kujifunza kwa makabili mengine namna ya kuhudumia akina mama waliojifungua kwa kuanza shughuli za kiuchumi baada ya miezi mitatu ya kujifungua badala ya wiki moja kama ambavyo wengi wao hufanya.
” Unakuta mama katoka kujifungua tuu ndani ya wiki anaenda shambani anamuweka mtoto chini ya mti wakati yeye akilima, sasa kwa mazingira hayo mnategemea huyo mtoto ananyonyeshwa na kuandaliwa lishe bora saa ngapi!?”. Amesema Mtaka.
Sanjali na hilo pia amewataka wazazi kuacha kuwalisha watoto viporo vya chakula ikiwemo viporo vya kande na kuwanyamazisha kwa kuwanywesha pombe ili walale usingizi kwani kwa kufanya hivyo ni kuwaharibu watoto kiafya na kiakili.
Naye mganga mkuu wa Mkoa wa Njombe Juma Mfanga amesema mkoa wa Njombe umetajwa kuwa nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 50.4 ya uwepo wa watoto wenye udumavu chini ya umri wa miaka mitano huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na mkoa wa Iringa ambao una asilimia 56.9.