Na Sophia Kingimali.
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo yote ya watahiniwa 102 waliofanya udanganyifu ikiwa pamoja na kuandika lugha za matusi kwenye karatasi za majibu.
Akitangaza matokeo hayo leo januari 25,2024 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA),Dk.Said Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 572,359 walisajiliwa kufanya mtihani
huo Novemba mwaka jana.
Dk.Mohamed amesema Baraza la Mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 102, mmoja akiwa wa maarifa na 101 wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ambao waliobainika kufanya udanganyifu katika Mtihani.
JUMLA ya watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha nne mwaka jana wamefaulu.
Dk.Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha nne mwaka jana wamefaulu ambapo kati yao wasichana waliofaulu ni 257,892 sawa na asilimia 86.17 huku wavulana wakiwa 226,931 sawa na asilimia 89.40.
Pia amesema mwaka 2022 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 476,450 sawa na asilimia 86.78 na kusababisha ufaulu wa watahiniwa kuongezeka kwa asilimia 0.87 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Dk.Mohamed amesema jumla ya watahiniwa wa Shule 471,427 kati ya 527,576 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 89.36 wamefaulu na kupata daraja la kwanza hadi la nne.
“Mwaka 2022 Watahiniwa waliofaulu walikuwa 456,975 sawa na asilimia 87.79. Hivyo, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.57 na kuna ongezeko la watahiniwa 14,452 sawa na asilimia 3.16 ya waliofaulu ikilinganishwa na mwaka 2022″amesema.
Amesema kati ya watahiniwa 471,427 waliofaulu, Wasichana ni 250,147 sawa na asilimia 88.11 na Wavulana ni 221,280 sawa na asilimia 90.81. Hivyo, Wavulana wamefaulu vizuri zaidi kuliko Wasichana.
Aidha akizungumzia watahiniwa wa kujitegemea Dk.Mohamed amesema watahiniwa wa Kujitegemea waliofaulu mtihani ni 13,396 sawa na asilimia 52.44.
“Mwaka 2022 Watahiniwa wa Kujitegemea 19,475 sawa na asilimia 68.34 walifaulu mtihani huo. Hivyo, ufaulu wa Watahiniwa wa Kujitegemea umeshuka kwa asilimia 15.90 ikilinganishwa na mwaka 2022″amesema.
Amesema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa Shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa Madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 197,426 sawa na asilimia 37.42.
Dk.Mohamed amesema mwaka 2022 watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 192,348 sawa na asilimia 36.95. Hivyo, ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.47 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Pia amesema ubora wa ufaulu wa Madaraja ya kwanza hadi tatu ni mzuri zaidi kwa wavulana ikilinganishwa na Wasichana ambapo Wavulana ni 108,368 sawa na asilimia 44.47 na Wasichana ni 89,058 sawa na asilimia 31.37.
Vilevile Baraza la Mitihani la Tanzania limezuia kutoa matokeo yawatahiniwa 376 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne, 2023 kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.
Pia watahiniwa watano wa mtihani wa taifa wa Kidato cha nne wamefutiw matokeo Kwa kuandika lugha ya matusi katika skripti zao.
“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani Mwaka 2016,” amesema.
Hata hivyo NECTA imezipogeza Kamati za Uendeshaji Mitihani za Mikoa na Halmashauri, Manispaa na Jiji, Wakuu wa Shule, Wasimamizi na Wasahihishaji wa mtihani huo Kwa kazi nzuri ya kutekeleza jukumu la uendeshaji mtihani huo.