Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa wakati akiwasili katika kiwanda cha ‘Tanzania Biotech Products ltd’ (TBPL) kilichopo Mkoani Pwani akiwa katika ziara yake ya siku Tatu nchini Tanzania.
Rais Salvador ametembelea Kiwanda hicho cha viuadudu vya kuuwa viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria (TBPL) jioni ya leo Januari 24, 2024 ambacho kimejengwa na Serikali ya Jamhuri ya Cuba na kuzinduliwa na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete Mwaka 2013 kwa lengo la kusisitiza jukumu muhimu la TBPL katika jitihada zinazoendelea za kutokomeza Malaria nchini.
Ziara hii inaashiria hatua muhimu katika ushirikiano wa kudumu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya watu wa Cuba katika jitihada za kutokomeza ugonjwa huo wa Malaria nchini.
Waziri Ummy ameshiriki ziara hiyo pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Anjera Kairuki, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge pamoja na viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya.