NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa ameupongeza utendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kufanya kazi kwa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kuleta tija kwa Taifa.
Akizungumza leo Januari 24, 2024 Jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi cha Waziri wa TAMISEMI, TARURA , Makatibu Tawala, Wasaidizi Miundombinu, Wakandarasi Wazawa, Wataalam pamoja na washauri wa Taasisi, Mhe.
Mchengerwa, amesema kuwa TARURA wamefanya kazi kubwa kwa kutengeneza barabara kwa kiwango la lami.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa ujenzi wa barabara wa kiwango cha lami umeongezeka kutoka kilometa 1,449.04 hadi kufikia kilometa 3, 224.12 sawa na ongezeko la asilimia 122.4.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changalawe umeongezeka kwa asilimia 98.44 kutoka kilometa 24, 405.4 hadi kufikia kilometa 41, 107.52.
“Hadi kufikia mwaka 2025 TARURA watakuwa wamejenga barabara kwa kiwango cha lami mjini na Vijiji kwa asilimia 85” amesema Mhe. Mchengerwa.
Ameeleza kuwa wataendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa
Wakandarasi Wazawa kwa kuwainua ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta ushindani kwa wakandarasi kutoka Mataifa mbalimbali.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, amesema kuwa kwa sasa wanatekeleza awamu ya pili ya mpango wa miaka mitano.
Mhandisi Seff amesema kuwa lengo ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025-2026 asilimia 85 ya mitandao ya barabara katika Wilaya zote nchini ziwe zinapitika.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 wametengewa shilingi bilioni 818 ambapo bilioni 710 ni fedha za ndani, huku bilioni 107.7 zinatoka kwa wadau wa maendeleo.
Mhandisi Seff amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2023 wamefanikiwa kutekeleza asilimia 38 kwa kufanya matengenezo ya barabara ya kawaida kilometa 21,000, lami kilometa 338, changalawe kilometa 8,546 pamoja na madaraja 4, 372.