…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wafanyabiashara wadogo maarufu kama (machinga) wametakiwa kuzingatia,kushiriki kikamilifu kwenye suala la usafi katika maeneo yao ya kazi hatua itakayosaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 24, 2024 na Afisa afya,elimu na uhamasishaji Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoani mwanza Rose Nyemele, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko jipya lililopo mtaa wa Nyanda Kata ya Nyasaka Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa juu ya kuzingatia usafi.
Nyemele amesema uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya biashara unasababisha magonjwa ya mlipuko ambayo yatawafanya washindwe kuendelea na biashara zao.
“Endeleeni kuzingatia taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya sanjari na kuwa na matumizi sahihi ya vyoo ili muweze kufanya kazi zenu katika mazingira salama,gharama ya kusafisha mazingira yenu ni kidogo ukilinganisha na gharama mtakazozitumia kwaajili ya matibabu”, amesema Nyemele.
Kwaupande wake Diwani wa Kata ya Nyasaka Wilaya ya Ilemela Mkoani mwanza Abdulrahman Simba, amewaomba wafanyabiashara kuweka Mpango kazi wa kushirikiana na wakala anaekusanya uchafu ili kuweka mazingira ya masoko kuwa rafiki.
“Lengo letu siyo kufunga minada tunahitaji watu wafanye kazi zao kwakuzingatia usafi ili waweze kujikwamua kiuchumi, afya ni mtaji hivyo zingatieni usafi kwa masilahi mapana ya uchumi wenu”, amesema Simba.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya vyoo vya soko hilo kufungwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo maji amewaomba wafanyabiashara kuendelea kutumia choo cha kulipia ambacho kipo katika maeneo ya Soko hilo wakati Serikali ya mtaa ikiendelea kufanya marekebisho.
Mponeja Igali ni Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Nyanda uliopo Kata ya Nyasaka Wilaya ya Ilemela Mkoani mwanza, amewasihi wafanyabiashara kushirikiana katika usafi ili wazidi kulinda mazingira yao ya kazi huku akiwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake.
Naye Mwenyekiti wa wajasiriamali, masoko na minada Mkoa wa Mwanza, ametoa ombi kwa Mtendaji na mwenyekiti wa mtaa wa Nyanda washirikiane na Polisi jamii kupanga utaratibu mzuri wa kulinda mazingira kwa baadhi ya wamachinga wanaochafua mazingira.
“Tujitahidi kufanya usafi wa mazingira tunayofanyia kazi ili tuendelee kuyalinda maeneo tuliyopewa na Serikali tusipozingatia msipozingatia usafi katika kipindi hiki cha mlipuko huu wa kipindupindu tunaweza kufungiwa kufanya biashara”, amesema Moniko
Annastazia Andrea ni miongoni mwa wafanyabiashara wa Soko jipya amesema anaendelea kuzingatia maelekezo anayopewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono na maji tiririka pamoja na kula chakula cha moto.