Na Issa Mwadangala wa Polisi Mkoa wa Songwe.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Isanzo iliyopo Kata ya Chapwa mjini Tunduma wametakiwa kunawa mikono kabla na baada ya kula ili kujilinda dhidi ya magonjwa ya milipuko.
Rai hiyo imetolewa Januari 24, 2024 na Mkaguzi Kata ya Chapwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Antony Sabasaba wakati alipokuwa anatoa elimu ya umuhimu wa kutunza mazingira na kuzingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kufunika chakula, maji na kuosha mikono kabla na baada ya kula kwa wanafunzi wa Shule hiyo.
“Utupaji wa takataka hovyo unaweza kupelekea kuibuka kwa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu ambacho huleta athari kubwa kwenye jamii” alisema Mkaguzi Sabasaba.
Mkaguzi Sabasaba alimtaka kila mwanafunzi wa Shule hiyo kuwa Balozi wa kumsimamia mwenzake ili kuweka mazingira safi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya usafi wanapokuwa nyumbani ili kuilinda jamii dhidi ya magonjwa yanayotokana na uwepo wa uchafu mtaani.